1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Bush anataka suluhisho la mzozo wa Mashariki ya Kati kabla kuondoka madarakani

26 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBf8

Rais George W Bush wa Marekani amesema anataka kupata suluhisho la mgogoro wa Mashariki ya Kati kabla kuondoka madarakani. Hayo yemesema na rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas kwenye mahojiano yake yaliyochapishwa hii leo.

Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, amesema wameanza mazungumzo ya maana na rais Abbas kuhusu mpango mpya wa amani na maswala yatakayosaidia kuundwa kwa taifa huru la Wapalestina. Olmert amesema, ´Hatufanyi hivyo kwa sababu ya upendo fulani, tunajaribu kufanya hivyo kwa sababu moja tu. Tunahitaji kutafuta mshirika kutoka upande ule mwingine kama tunataka kutazamia kujenga siku nzuri za usoni.´

Sambamba na hayo mjumbe wa pande nne zinazoudhamini mpango wa amani ya Mashariki ya Kati, Tony Blair, anazuru jumuiya ya falme za kiarabu.

Jumuiya hiyo imesema wakati umewadia kwa juhudi za maana zifanywe kufikia amani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa jumuiya ya famle za kirabu, Sheikh Abdullah bin Zayed al Nahayan, amesema anamuunga mkono Tony Blair kama mjumbe maalumu wa Mashariki ya Kati kuendeleza mchakato wa kutafuta amani baina ya Israel na Wapalestina.