1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Ehud Olmert ataka mkutano na viongozi wa kiarabu

2 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDG

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert amesema kwamba yuko tayari kuhudhuria mkutano na viongozi wa kiarabu kujadili mpango wa amani uliopendekezwa na Saudia.

Olmert ametoa tamko hilo wakati alipowahutubia waandishi wa habari akiwa pamoja na kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Bibi Merkel awali alikutana na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah ambako aliwaeleza waandishi wa habari kwamba ana imani kuwa nafasi bado ipo ya kufufua mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati yaliyokwama.

Kansela wa Ujerumani ambae anafanya ziara yake ya kwanza katika eneo la mashariki ya kati kama rais wa nchi za umoja wa ulaya amesema kuwa umuhimu mkubwa unastahili kutolewa katika kuafikia suluhisho la kuwepo madola mawili ambako Palestina huru itaweza kuwa jirani wa Israel katika hali ya amani na utulivu.

Bibi Merkel anatarajiwa kuwasili nchini Lebanon asubuhi leo kukutana na waziri mkuu Fuad Siniora, atakutana pia na spika wa bunge na kiongozi wa upinzani Nabih Berri kisha viongozi hao watawahutubia waandishi wa habari.

Wakati huo huo mkuu wa sheria wa Israel amesema kuwa anapanga kuongeza kosa jingine la ubakaji katika kesi dhidi ya rais Moshe Katsav wa Israel.

Tangazo hilo limetokea baada ya mlalamikaji mpya

Kujitokeza, mwanamke huyo amedai kwamba rais Katsav alimbaka katika afisi zake wakati alipokuwa waziri wa utalii mnamo miaka ya 90.

Uamuzi iwapo rais Moshe Katsav atafunguliwa mashtaka utatolewa tarehe 2 mwezi wa tano.