1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Merkel aendelea za ziara yake ya Mashariki ya Kati

1 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDS

Kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, ameanza mazungumzo na viongozi wa Israel na Palestina hii leo kama sehemu ya juhudi za kuufufua mchakato wa kutafuta amani baina ya Israel na Palestina. Hata hivyo wapambe wa kansela Merkel wamesema kiongozi huyo hatakutana na baadhi ya wanachama wa serikali mpya ya umoja wa taifa ya mamlaka ya Palestina.

Kansela Merkel, ambaye nchi yake ni rais wa Umoja wa Ulaya, anajaribu kuendeleza kasi ya mazungumzo ya kutafuta amani ya Mashariki ya Kati kufuatia mkutano wa kilele wa viongozi wa kiarabu uliofanyika mjini Riyadh Saudi Arabia wiki iliyopita. Kiongozi huyo hata hivyo amekiri juhudi zake zinakabiliwa na vikwazo.

Kansela Merkel amefanya mazungumzo na waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel, Tzipi Livni, mjini Jerusalem mapema leo kabla kulitembelea jumba la makumbusho ya mauaji ya halaiki ya Wayahudi la Yad Vashem.

Baadaye leo anatarajiwa kukutana na rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, mjini Ramallah huko Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan kabla kurejea Jerusalem kwa mazungumzo zaidi na waziri mkuu Ehud Olmert.