1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Mkutano wa kilele wa Mashariki ya Kati kufanyika leo

19 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCQl

Mkutano wa kilele kuhusu Mashariki ya Kati utafanyika leo mjini Jerusalem nchini Israel. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, ambaye yumo mjini Jerusalem kuhudhuria mkutano huo, ana matumaini ya kuyajadili maswala muhimu yanayokwamishwa na serikali mpya ya Palestina itakayoundwa.

Uwezekano ni mdogo wa serikali ya umoja wa taifa itakayoundwa na chama cha Hamas na Fatah kuitambua kikamilifu Israel. Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, amesema Israel na Marekani zimekubaliana kutoitambua serikali mpya ya Palestina itakayoshindwa kuyakomesha machafuko, kukataa kuitambua Israel na kushindwa kuikubali mikataba ya amani iliyopo.

Mkutano wa leo mjini Jerusalem hautarajiwi kuleta matumaini kwa sababu ya hali ya kisiasa katika maeneo ya Wapalestina na udhaifu wa serikali ya Israel.

Hapo jana rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, alijaribu kumsihi Condoleezza Rice aipe nafasi serikali mpya ya Hamas na Fatah katika mkutano uliofanyika mjini Ramallah huko Ukingo wa magharibi wa mto Jordan.

Condoleezza Rice amesema Marekani haitabadili msimamo wake wala kupitisha uamuzi wowote mpaka serikali mpya ya Palestina itakapoundwa.