1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM : Olmert akutana na Abbas

24 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCgc

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina wamekuwa na mazungumzo yao ya kwanza rasmi hapo jana na kukubaliana kujaribu kufufuwa mazungumzo ya amani yaliosambaratika hapo mwaka 2000.

Olmert amemwambia Abbas kwamba ataachilia mapato ya kodi ya Wapalestina ya dola milioni 100 aliyoyazuwiya na kuondowa baadhi ya vizuizi kwenye Ukingo wa Magharibi lakini hakuna usuluhishi uliofikiwa katika suala la kuwaachilia wafungwa wa Kipalestina au kutanuwa usitishaji tete wa mapigano wa Gaza hadi Ukingo wa Magharibi.

Olmert amekuwa chini ya shinikizo la Marekani na Umoja wa Ulaya kuchukuwa hatua za kumuunga mkono Abbas kutokana na wito wake wa kuitisha uchaguzi na mapema ambao kundi la Hamas linaloongoza serikali ya Palestina limeukataa kwa kusema kuwa ni kutaka kufanya mapinduzi dhidi ya serikali hiyo na pia ni kinyume na katiba.

Katika mazungumzo rasmi kati ya viongozi hao wawili kufanyika takriban baada ya kipindi cha miaka miwili Olmert na Abbas wamekubaliana kuwa na mikutano kadhaa katika siku za usoni kwa lengo la kujaribu kufufuwa mazungumzo ya amani.