1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jerusalem. Viongozi wataka ushirikiano zaidi. Mogadishu. Mapigano yanaendelea.

24 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCgR

Mapigano nchini Somalia kati ya majeshi ya serikali yanayosaidiwa na majeshi ya Ethiopia na yale ya jeshi la mahakama za Kiislamu yameingia katika siku ya tano na kusambaa katika miji mingine miwili kiasi cah kilometa 300 kaskazini ya Mogadishu. Pande zote mbili zimesema kuwa mapigano yamekuwa makali katika miji ya Beledweyne na Bindiradley lakini hazikutoa maelezo zaidi kuhusu watu walioathirika.

Milio ya makombora pia imesikika karibu na Baidoa, mji ambao una makao rasmi ya serikali ya Somalia.

Mapigano yamezuka Jumatano wili iliyopita baada ya kumalizika kwa muda uliotolewa na mahakama za Kiislamu kwa majeshi ya Ethiopia kuondoka nchini humo. Ethiopia inakana kuwa majeshi yake yanahusika katika mapigano hayo, ikisema kuwa imetuma tu wataalamu wanaofundisha jeshi la nchi hiyo.

Majeshi ya mahakama za Kiislamu yanadhibiti mji mkuu Mogadishu na baadhi ya maeneo ya Somalia.

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na rais wa Palestina Mahmoud Abbas wamekubaliana kuendeleza hatua za kuleta amani kati ya Israel na mamlaka ya Wapalestina wakati walipokutana mjini Jerusalem.

Kiongozi huyo wa Israel alikubali kutoa kiasi cha dola milioni 100 zilizozuiwa kwa rais wa Palestina Mahmoud Abbas na kupunguza vikwazo vya kusafiri kwa watu wa eneo la ukingo wa magharibi.

Ofisi ya waziri mkuu Olmert imeuita mkutano huo kuwa ni hatua ya kwanza kuelekea kujenga uaminifu baina ya pande hizo na ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Maafisa wa Palestina wamesifu hali ya uchangamfu katika mazungumzo hayo na kusema mikutano zaidi inapangwa kufanyika.