1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM: Wapatanishi wa mashariki ya kati wakutana leo

26 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBoA

Wapatanishi wa mzozo wa mashariki ya kati wamekutana mapema leo mjini Jerusalem nchini Israel. Mkutano huo umefanyika siku moja baada ya viongozi wa Israel, Palestina, Misri na Jordan kuahidi kushirikiana kuufufua mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

Mkutano huo uliowaleta pamoja wajumbe wa pande nne zinazoudhamini mpango wa amani ya mashariki ya kati kutoka Marekani, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Urusi ni wa kwanza tangu kundi la wanamgambo wa kiisilamu la Hamas liliponyakua madaraka katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Pande hizo nne zinatarajiwa kumtaja waziri mkuu wa Uingereza anayeondoka Tony Blair kama mpatanishi mkuu katika mgogoro wa mashariki ya kati. Msemaji wa ubalozi wa Uingereza mjini Jerusalem, Karen Kaufman, hakuthibitisha ripoti hiyo.

Waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuhudhuria mkutano huo uliofanyika katika ubalozi mdogo wa Marekani mjini Jerusalem.