1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la anga la Libya lazidi kurudi nyuma

Kabogo Grace Patricia24 Machi 2011

Kamanda wa juu wa Uingereza amesema kuwa vikosi vya jeshi la muungano vimekiangamiza kikosi cha jeshi la anga la Libya. Jemadari Greg Bagwell amesema ndege za vikosi hivyo sasa zinaruka kwa uhuru kuzunguka Libya.

https://p.dw.com/p/10ga8
Moja ya ndege za Uingereza zilizokwenda LibyaPicha: AP

Mashambulizi yanawalazimisha wanajeshi watiifu kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi kurudi nyuma, ingawa bado wanashambulia kambi za waasi katika miji ya Misrata ulioko magharibi na Adjabiya ulioko mashariki.

Kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kimetangaza kuwa kikosi hicho cha muungano wa kimataifa kinaendelea na mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya Kanali Gaddafi kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Schweiz Wirtschaft Weltwirtschaftsforum in Davos Großbritannien David Cameron
Waziri Mkuu wa Uingereza, David CameronPicha: dapd

Wakati huo huo, Uingereza imetangaza kuandaa mkutano wa kimataifa utakaojadili maendeleo ya kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Libya. Mkutano huo utakaofanyika Jumanne ijayo mjini London, utalenga zaidi kuhusu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na mahitaji ya kibinaadamu ya watu wa Libya.

Bado haijafahamika jukumu ambalo Jumuiya ya Kujihami ya NATO italitimiza katika kutekeleza operesheni ya kuzuia ndege kuruka kwenye anga ya Libya, ambayo kwa sasa inaongozwa na Marekani. Rais Barack Obama wa Marekani anataka kukabidhi jukumu hilo haraka iwezekanavyo. Wiki iliyopita, Ujerumani haikupiga kura katika baraza hilo la usalama.

Deutschland Bundestag Verteidigungsminister Thomas de Maiziere
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Thomas de MaizierePicha: dapd

Aidha, juzi Jumanne Ujerumani ilijiondoa katika operesheni za NATO kwenye Bahari ya Meditteranean kutokana na jumuiya hiyo kujiingiza katika mzozo wa Libya na kurejesha udhibiti wa meli nne za kijeshi chini yake. Lakini katika hatua ya kukisaidia kikosi cha muungano nchini Libya, baraza la mawaziri la Ujerumani jana lilipitisha mipango ya kupeleka wanajeshi wa kurusha ndege za uchunguzi za NATO nchini Afghanistan.