1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Iraq lawakomboa wafungwa 1,500 wa IS

Mohammed Khelef3 Aprili 2016

Vikosi vya jeshi la Iraq vimewakomboa wafungwa zaidi ya 1,500 kutoka gereza kubwa la chini ya ardhi lililokuwa likimiliwa na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu baada ya kuuchukuwa mji wa magharibi mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1IObW
Wanajeshi wa Iraq baada ya kuukomboa mji wa Heet uliokuwa mikononi mwa IS.
Wanajeshi wa Iraq baada ya kuukomboa mji wa Heet uliokuwa mikononi mwa IS.Picha: Getty Images/AFP/M. Al-Dulaimi

Maafisa wanasema jeshi limezitwaa baadhi ya sehemu za mji wa Heet, ambao ni kati ya sehemu zenye wakaazi wengi zaidi katika jimbo la Anbar linaloendelea kushikiliwa na kundi hilo la kigaidi kwa kiasi kikubwa.

"Wakati wakisonga mbele na kuurejesha mji wa Heet kutoka kwa Daesh (jina linalotumika kuwaita magaidi wa IS), wanajeshi waliweza kugundua gereza moja kubwa," Kanali Fadhel al-Nimrawi aliwaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa gereza hilo lilikuwa chini ya ardhi.

Malallah al-Obeidi, afisa kwenye jimbo la Anbar, pia alisema idadi ya wafungwa waliokuwamo kwenye gereza hilo walikuwa 1,500, huku wengi wao wakiwa raia.

Kundi la IS limekuwa likiyashikilia maeneo makubwa ya kaskazini na magharibi mwa Iraq tangu mwaka 2014, ingawa katika siku za hivi karibuni vikosi vya serikali vimekuwa vikipata mafanikio machache dhidi ya magaidi hao.

Baada ya kutwaliwa kwa mji mkuu wa Anbar, Heet na Fallujah yalikuwa ni maeneo mawili yenye idadi kubwa zaidi ya watu ambayo yalikuwa bado yakishikiliwa na IS katika jimbo hilo.

Jeshi la Iraq lilianza operesheni kubwa ya kuutwaa mji wa Heet katikati ya mwezi Machi, lakini idadi kubwa ya wanajeshi wakalazimika kurejea kwenye mji mkuu Baghdad kwa muda kuwalinda maelfu ya waandamanaji wanaoishinikiza serikali ya Waziri Mkuu Haider Abadi kufanya mageuzi ya baraza la mawaziri.

Jeshi la Syria lagundua kaburi la pamoja

Hayo yakiendelea, nako Syria jeshi limegundua kaburi moja lililozikwa watu 42 kwa pamoja, ambao inaaminika waliuawa na kundi la Dola la Kiislamu.

Sehemu ya magofu ya Palmyra yaliyobomolewa na IS kabla ya kukombolewa na jeshi la Syria.
Sehemu ya magofu ya Palmyra yaliyobomolewa na IS kabla ya kukombolewa na jeshi la Syria.Picha: Getty Images/AFP/J. Eid

Siku kadhaa baada ya wanajeshi hao kuutwaa tena mji wa Palmyra kutoka mikononi mwa IS, serikali inasema maafisa wa jeshi wamegundua kaburi hilo likiwa wamezikwa "maafisa wa serikali, wanajeshi, wapiganaji wanaounga mkono serikali na jamaa zao."

Chanzo kimoja jeshini kililiambia shirika la habari la AFP kwamba 24 kati ya maiti zilopatikana kwenye kaburi hilo ni raia, wakiwemo watoto watatu, ambao waliuawa "aidha kwa kukatwa vichwa au kupigwa risasi."

Jumapili iliyopita (27 Machi), jeshi la Rais Bashar al-Assad lilifanikiwa kuukomboa mji huo wa kale ulio kwenye hifadhi ya Shirika la Utamaduni, Elimu na Sayansi la Umoja wa Mataifa (UNESCO), baada ya kuwa mikononi mwa IS tangu Mei 2015.

Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake London, ndani ya kipindi cha miezi 10 cha kuukalia mji huo, "IS iliuwa raia wapatao 280, miongoni mwao wanajeshi 25 waliowauwa kwenye ukumbi wa maonesho ya Kirumi muda mchache baada ya kuutwaa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Yusra Buwayhid