1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Kenya laishambulia al-Shabab Somalia

Ambia Hirsi24 Desemba 2015

Ndege za kivita za Kenya zimeshambulia ngome ya kundi la waasi wa al-Shabaab karibu na mji wa bandari ya kusini ya Kismayo usiku wa Jumatano, huku duru zikisema kwamba raia sita wameuawa.

https://p.dw.com/p/1HTMn
Jeshi la Kenya nchini Somalia
Jeshi la Kenya nchini SomaliaPicha: Reuters

Makombora yaliyorushwa na wanajeshi hao yaliharibu ngome kadhaa za waasi hao. Wakaazi wa eneo hilo waliozungumza na shirika la habari la dpa, walisema askari wenye silaha wa Somalia walishika doria katika kijiji cha Berhani baada ya shambulizi hilo.

Kwa mujibu wa Abdinasir Seerar, ambaye ni msemaji wa utawala wa mkoa katika eneo la Jubaland, askari wa Somalia waliteka kijiji cha Berhani kutoka kwa al-Shabaab, na kuwaua wanamgambo kadhaa.

Seerar aliongeza kuwa wanajeshi wa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa Afrika kutoka Kenya waliwasaidia maafisa wa usalama wa Somalia kufanya mashambulizi amabayo ni hatua muhimu katika juhudi za kutwaa maeneo yanayokaliwa na wanamgambo hao katika maeneo ya kusini. Msemaji huyo hata hivyo alikataa kutoa taarifa zozote iwapo raia waliuawa wakati wa oparesheni hiyo.

Vikosi vyashirikiana Berhani

Maafisa wa jeshi la Kenya washika doria
Maafisa wa jeshi la Kenya washika doriaPicha: AP

Kijiji cha Berhani, kilichoko umbali wa kilomita 78 kaskazini magharibi mwa mji wa bandari wa Kisimayu kwa muda mrefu kimekuwa chini ya udhibiti wa al-Shabaab. Mnamo Jumanne vikosi vya Umoja wa Afrika kwa ushirikiano na vikosi vya Somalia walifanikiwa kutwaa kijiji Aw-dheegle katika mkoa wa Shabelle ya Chini, huku makamanda wa kijeshi wa Somalia wakithibitisha kuwaua wanamgambo wasiopungua watano katika makabiliano hayo.

Huku hayo yakijiri wanamgambo wa kundi la al-Shabaab jana waliwanyonga hadharani afisa mmoja wa jeshi la Somalia pamoja na kiongozi wa mji mdogo kusini mwa mkoa wa Shabelle. Kundi hilo ambalo linataka kuipindua serikali inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa limekuwa likipania kulazimisha kutekelezwa kwa sheria kali za Kiislamu, linasalia kuwa kitisho kwa usalama katika taifa hilo la pembe ya Afrika baada ya kutimuliwa kutoka mji mkuu wa Mogadishu mwaka 2011.

Vikosi vya kulinda usalama vya Umoja wa Afrika kwa ushirikiano na jeshi la Somalia vimepata mafanikio makubwa dhidi ya kundi la al shabab, lakini wanamgambo hao bado wanadhibiti baadhi ya maeno ya chini ya Shabelle, ingawa wamekuwa wakisukumwa nje ya miji ya katikati ya mji wa bandari wa Kisimayu.

Taifa la Somalia,ambalo lilitumbukia kwenye machafuko baada ya dikteta Mohamed Siad Barre kung'olewa mamlakani mwaka 1991, liko katika harakati za kujijenga upya baada ya miongo miwili ya migogoro na machafuko.

Mwandishi: Ambia Hirsi/DPAE/RTRE

Mhariri:Iddi Ssessanga