1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Kongo lashambulia ngome ya Nkunda.

3 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CWJX

Kigali. Jeshi la jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo limeshambulia ngome ya jenerali muasi Laurent Nkunda, likitumia makombora kama sehemu ya operesheni iliyotarajiwa kuwaondoa waasi hao katika eneo hilo.

Msemaji wa umoja wa mataifa meja Vivek Goyal amesema kuwa majeshi hayo yamefanya mashambulizi hayo katika eneo la Mushake. Wapiganaji wanaomuunga mkono jenerali Nkunda hata hivyo wamesema wamekamata miji ya Kikuku na kituo muhimu cha jeshi katika mji wa Nyanzale jana Jumapili, shambulio ambalo limesababisha watu 40,000 kukimbia makaazi yao.

Duru za wanaharakati wa haki za binadamu zinasema kuwa Nyanzale unakaliwa na wakaazi karibu 30,000 hadi 40,000 ambao wamekimbia mapigano kutoka sehemu nyingine nchini humo, lakini wamesema kuwa simu katika mji huo hazifanyi kazi kwa hiyo ni vigumu kuthibitisha jinsi raia wanavyoishi katika eneo hilo.