1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Kongo lazima jaribio la M23 kuutwaa mji wa Sake

8 Februari 2024

Jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linasema limezima jaribio la waasi wa M23 waliokuwa wamekaribia kuutwaa mji wa Sake, huku watu saba wakiuawa baada ya bomu kuangukia eneo la makaazi kwenye mji huo.

https://p.dw.com/p/4cA4N
Jeshi la Kongo
Jeshi la KongoPicha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Taarifa zinasema kuwa jeshi la Kongo lilitumia ndege za kivita kuwasambaratisha wapiganaji wa kundi hilo waliokuwa tayari wameukaribia mji wa Sake, ambamo walikua wameanza kurushia makombora.

Baadhi ya raia waliukimbia mji huo kufuatia miripuko ya mabomu, lakini wengine waliamua kubakia majumbani mwao na kufikia asubuhi ya Alkhamis, DW iliwashuhudia wakiendelea na shughuli zao baada ya kurejea kwa utulivu mdogo.

Soma zaidi: Jeshi la DR Kongo lawazuiwa waasi wa M23 kuutwaa mji wa Sake

"Nipo hapa Sake nauza unga wa mihogo na sioni tatizo lolote kabisa", alisema mmoja wao na mwengine aliongeza: "Tupo hapa tunauza dagaa lakini tatizo ni kwamba hatuwapati wateja sababu sote tumekuwa wakimbizi."

Mwengine aliiambia DW kwamba "Habari zinazozagaa kwamba wanajeshi wetu wamekimbia ni uongo mtupu. Sisi kama raia hatutawaachilia kamwe askari wetu." 

DR Kongo | M23
Mmoja wa wapiganaji wa kundi la waasi la M23 mashariki mwa Kongo.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Raia waapa kubakia Sake

Gilbert Bahati, mkaazi wa eneo hilo aliapa kutokuuacha mji huo licha ya kufariki kwa watu saba waliongukiwa na bomu wakati wa mapigano  hayo baina ya jeshi la serikali na wapiganaji wa M23  kwenye vijiji vya Malehe na Kihuli, umbali wa kilomita 6 kutoka Sake. .

"Sisi hatuwezi kuuacha mji wetu huu na hapa ndipo tutafariki. Sisi vijana tupo tayari kulisaidia jeshi pamoja na Wazalendo ili wawe na uwezo wa kuulinda mji wetu." Alisema kijana huyo.

Soma zaidi: Wanne wauawa, 25 wajeruhiwa kwa mabomu ya M23

Kwa upande wake, gavana wa kijeshi kupitia msemaji wake wa kiraia, Jymi Nziali, aliyeuzuru mji wa Sake jioni ya Jumatano (Februari 7), aliviambia vyombo vya habari kuwa hali ni tulivu hadi asubuhi ya Alkhamis na kuwa wanachi walikuwa wameanza sasa kurejea majumbani mwao.

"Raia wako hapa kama mnavyowaona, pia wanajeshi wetu wanafanya ulinzi wa mji. Kwa hiyo, Jenerali Chirimwami, gavana wa jimbo, anawaomba wananchi kuwa watulivu na kuwa na uhakika kwamba jeshi linafanya kila liwezekanalo ili kulinda mji wa Goma, Sake pia na maeneo mengine ya Kivu kaskazini." Alisema gavana huyo.

DR Kongo | Wazalendo
Baadhi ya vijana wa kundi lijiitalo "Wazalendo" ambao wanaungwa mkono na jeshi la Kongo kwenye vita dhidi ya kundi la M23.Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mapigano makali Nyiragongo

Hata hivyo, ripoti zilisema kuwa mapigano mengine makali yalikuwa yanaendelea hadi mchana wa Alkhamis kwenye mji wa Kibumba wilayani Nyiragongo ulio umbali wa kilomita 22 kaskazini mashariki mwa mji wa Goma, ambako wapiganaji vijana wanaojiita Wazalendo na wanaoungwa mkono na jeshi la Kongo wanakabiliana na M23. 

Soma zaidi: Jeshi la DRC lapambana na M23 Kivu Kaskazini

Raia eneo hilo wameeleza kusikia milio ya makombora tangu asubuhi ya Alkhamis wakati vijana Wazalendo walipokuwa wakizilenga kwa roketi ngome za M23 kwenye vijiji vya Rwibiranga na Ruhunda mbali kidogo na Kibumba ya Kati. 

M23 walirudi katika eneo hilo muda mfupi baada ya kuondoka kwa kikosi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama ilivyotakiwa na utawala wa Kinshasa.