1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la kulinda amani kupelekwa Afrika ya Kati

11 Oktoba 2013

Baraza la Usalama limepitisha kwa kauli moja azimio linaloutaka Umoja wa Mataifa kuzingatia kuliunda jeshi lenye uwezo kamili la kulinda amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa

https://p.dw.com/p/19xrz
Picha: P.Pabandji/AFP/GettyImages

Nchi hiyo yenye utajiri wa madini, ilitumbukia katika mgogoro tangu waasi wa kaskazini mwa nchi Seleka walipoutwaa mji mkuu Bangui, na wakamwondoa Rais Francois Bozize mwezi Machi.

Balozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati katika Umoja wa Mataifa Charles Armel Doubane ameliambia baraza la Usalama baada ya kura hiyo kuwa “uamuzi huo unatoa mwangaza wa matumaini kwa wanaume, wanawake na watoto milioni 4.6 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius, alionya kuwa Jamhuri ya Afrika ya Kati inakabiliwa na kitisho cha kutumbukia katika mgogoro kama wa Somalia kama haitapata msaada wa dharura.

Azimio hilo lililopitishwa na baraza la Usalama lenye nchi 15 wanachama linatoa wito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoa ripoti katika siku 30 ambayo itafafanua uwezekano wa msaada wa kimataifa kwa ujumbe utakaoundwa wa Umoja wa Afrika katika Afrika ya Kati unaofahamika kama MISCA. Ujumbe huo wa MISCA utakuwa na chaguo la kugeuzwa kuwa operesheni ya Kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, kwa kuzingatia namna mazingira yatakayokuwa nchini humo. Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Gerard Araud amewaambia wanahabari kuwa changamoto zitakuwa kubwa. Hivyo basi wazo ni kuwa jeshi la Afrika litatoa msaada mkubwa kwa juhudi za serikali ya Afrika ya Kati kurejesha himaya ya nchi.

Aliyekuwa kiongozi wa waasi Michel Djotodiaakila kiapo kama Rais mpya wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Aliyekuwa kiongozi wa waasi Michel Djotodiaakila kiapo kama Rais mpya wa Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: STR/AFP/Getty Images

Baraza hilo limeelezea hofu kuhusu “ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadaamu na ongezeko la ukiukaji wa haki za binadamu na mateso hasa kutoka kwa waasi wa Seleka”, na likadai kuwa waasi wa Seleka na makundi mengine yaweke chini silaha zao maramoja. Rais wa Jamhuri ya Afrika ya kati Michel Djotodia mapema mwezi huu alifanya mkutano na wanahabari mjini Bangui na kusema nchi yake haihitaji msaaada wa jumuiya ya kimataifa kutatua mizozo yake kwani wana njia za kushughulikia masuala ya ndani ya nchi hiyo. "Hatuhitaji usaidizi wowote kutoka jumuiya ya kimataifa.Tunaweza kuwashughulikia hao majangili na hicho ndicho tutafanya.Tumewapa miezi mitatu tu ya kujadiliana na wanafahamu hiloTunajua walipo majangili hao na tumeamua kukabiliana nao na tutapigana nao"

Tangu Rais Djotodia achukue madaraka baada ya Francois Bozize katika mapinduzi ya kijeshi, taifa hilo halijajua amani na mahitaji ya kibinadaamu yamekuwa yakiongezeka. Umoja wa Afrika ulikuwa umeomba msaada wa kifedha, kimiundo mbinu na kiufundi, kutoka kwa Umoja wa Mataifa, na maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wamependekeza Baraza la Usalama liidhinishe ombi hilo

Baadhi ya wajumbe wa nchi za magharibi wanasema hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ni tete ambayo haiwezi kuruhusu kutumwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika siku za karibuni. Maafisa wa Umoja wa Mataifa na wanadiplomasia wanasema mgogoro wa Afrika ya Kati umeshindwa kupata uungaji mkono wa kimataifa, kwa sababu umegubikwa na migogoro kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria. Wakati Umoja wa Afrika ukipanga kupeleka wanajeshi 3,600 wa kulinda amani katika ujumbe huo wa MISCA, nao wanajeshi wengine 1,100 wa kikanda wakiwa tayari nchini humo, inaonekana kuwa vigumu kwa mpango huo kuanza kufanya kazi kabla ya mwaka wa 2014.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Josephat Charo