1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Mali lapambana na waasi wa Tuareg, Kidal

19 Mei 2014

Mali imevituma vikosi kuukomboa mji wa Kaskazini mwa nchi hiyo Kidal, kutoka mikononi mwa waasi wa Tuareg baada ya wafanyakazi 6 wa serikali na raia 2 kuuawa, kufuatia shambulizi katika ofisi za Gavana wa jimbo hilo

https://p.dw.com/p/1C2F1
Mali Regierungschef Moussa Mara
Picha: AFP/Getty Images

Waasi hao wa Tuareg pia wamewateka nyara watu 30. Shambulizi hilo limemfanya Waziri Mkuu wa Mali Moussa Mara kutangaza vita dhidi ya wanamgambo hao. Karibu wanajeshi wanane waliuawa huku wafanyakazi wa umma 30 wakichukuliwa mateka na waasi baada ya mapigano kuzuka wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Moussa Mara katika mji huo wa kaskazini mwa Mali.

Msemaji wa waasi hao wanaopigania kujitenga amekanusha kuwa kuna yeyote aliyeuawa ndani ya jengo hilo la serikali. Mara amewaambia waandishi wa habari baada ya kuwasili Gao, mji mwingine wa Kaskazini, kuwa serikali tayari imevituma vikosi vyake, wakiwemo wanajeshi maalum, kuukomboa mji wa Kidal. Amesema magaidi wametangaza vita dhidi ya serikali, hivyo Mali iko vitani na magaidi. Waziri wa Ulinzi wa Mali Soumeylou Boubeye Maiga amesema wanajeshi wa serikali wamechukua udhibiti wa majengo yote ya serikali, isipokuwa tu ofisi za gavana, ambazo bado zimeshikiliwa na waasi.

Mara alikuwa akiuzuru mji huo, ambao ni ngome ya waasi wa Tuareg, kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa mwezi uliopita kama sehemu ya juhudi za kuyafufua mazungumzo yaliyochelewa ya amani na makundi yenye silaha kaskazini mwa nchi hiyo. Mara ameyakosoa majeshi ya Ufaransa na Umoja wa Mataifa kwa kuliwacha shambulizi hilo kufanyika. Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, kimesema askari wake 21 walijeruhiwa katika mapambano hayo wakati wakiweka ulinzi kwa ziara hiyo ya Waziri mkuu mjini Kidal. Haikubainika mara moja kama wanajeshi wa Ufaransa walihusika katika matukio hayo ya mwishoni mwa wiki mjini Kidal.

Waasi wa Tuareg wanataka uhuru wa eneo la kaskazini mwa Mali
Waasi wa Tuareg wanataka uhuru wa eneo la kaskazini mwa MaliPicha: Ollo Hien/AFP/Getty Images

Marekani imetoa wito wa pande husika kujizuia na kuwachiliwa huru mara moja kwa mateka hao. Imesema pande zote mbili zinastahili kutojihusisha na vitendo vitakavyohatarisha maisha ya mwananchi wa kawaida. Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani imesema njia pekee ya kupatikana amani ni kupitia mazungumzo.

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi – ECOWAS, yenye nchi 16 wanachama, pia imelaani machafuko hayo pamoja na “kuzorota pakubwa kwa hali ya kisiasa na usalama”. Serikali ya Mali imesema vurugu hizo zimesababishwa na waasi wa Tuareg wanaopigania kujitenga upande wa mashariki mwa nchi, lakini Waziri Mkuu Mara amesema makundi ya wanamgambo yanaitumia fursa ya mzozo uliopo ili kujipenyeza mjini Kidal, ili kushiriki katika machafuko hayo pamoja na makundi mengine ya kigaidi.

Baada ya kurejea mjini Bamako jana usiku, Mara amesema maafisa wanaendelea na juhudi za kuwezesha kuwachiliwa huru mateka hao. Amesema wengine “wameuawa kinyama, huku wengine wakiwachiwa huru kwa sababu ya majeraha waliyoyapata katika makabiliano hayo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mwandishi: Josephat Charo