1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Niger kwenda Nigeria

Admin.WagnerD11 Februari 2015

Bunge la Niger limeidhinisha kwa kauli moja hatua ya kutuma wanajeshi wake Kaskazini mwa Nigeria, kama sehemu ya -operesheni ya kijeshi ya nchi kadhaa za Afrika Magharibi, kupambana na waasi wa kundi la Boko Haram.

https://p.dw.com/p/1EZTD
Karte Nigeria Niger Boko Haram
Ramani ya Nigeria katika maeneo yanayokaliwa kwa kiasi kikubwa na wanamgambo wa Boko Haram

Kundi hilo la itikadi kali ya Kiislamu limeimarisha hujuma zake kwa mashambulizi kadhaa kwenye mpaka wa Niger na Nigeria na pia Cameroon katika wiki zilizopita.

Wabunge wote 102 wa bunge la taifa la Niger waliidhinisha hatua hiyo ya kutuma wanajeshi kaskazini mwa nchi jirani ya Nigeria, katika kura iliopigwa jana mjini Niamey. Spika wa bunge hilo Adamou Salifou alisema Niger itachangia bila ya shaka yoyote kupambana na kile alichokiita unyama unaofanywa na Boko Haram.

Katika siku chache zilizopita, Niger imekusanya wanajeshi zaidi ya 3,000 mjini Diffa katika mpaka wake wa Kusini mashariki na Nigeria, wakisubiri amri ya kusonga mbele.

Makubaliano ya mataifa Manne

Nigeria, Niger, Chad na Benin zilikubaliana mwishoni mwa juma lililopita kutuma kikosi cha wanajeshi 8,700 kupambana na Boko Haram , kundi ambalo limewauwa maelfu ya watu na kuwateka nyara mamia wengine katika kampeni ya vita vyake vya jihadi yenye lengo la kutaka kuunda dola la Kiislamu kaskazini mwa Nigeria.

Soldaten aus dem Tschad Archiv 2014
Wanajeshi wa Chad wakiwa katika operesheni.Picha: AFP/Getty Images/M. Medina

Nigeria imelazimika kuahirisha uchaguzi wa rais tarehe 14 ya mwezi huu wa Februari kwa muda wa wiki sita, ikielezwa kwamba ni kwasababu ya hali mbaya ya usalama.

Wakati huo huo milio ya risasi na makombora ilisikika jana usiku katika mji wa N´Guigmi katika mpaka wa Niger na Nigeria na taarifa ziliashiria kwamba huenda yalikuwa ni mapigano kati ya waasi wa Boko Haram na jeshi la Niger. Mji huo uko karibu na mto Chad kiasi ya kilomita 100 mashariki mwa Diffa,ambako mnamo siku ya Jumatatu watu watano waliuwawa katika shambulizi la bomu la kujilipua,likiwa la tatu katika muda wa siku nne.

hapo jana wakaazi wengi wa Diffa walionekana wakigombania kupata usafiri wa mabasi kuhama mji huo.

Duru kadhaa za usalama zilionya kwamba wapiganaji waliokuwa wakiishi miongoni mwa raia kaskazini mwa Nigeria, ni miongoni mwa watu waliokimbilia nchi jirani ya Niger na Waziri wa ulinzi wa Niger Karidio Mahamadou aliiambia stesheni moja ya redio ya binafsi kwamba hali mjini Diffa ni mbaya sana .

Kwa upande mwengine wahudumu wa misaada kutoka Shirika la kimataifa la msalaba mwekundu na lile la nchini Cameroon, wamesafiri kwenda eneo la mbali la kaskazini mwa Cameroon kujaribu kuboresha shughuli ya utoaji misaada kwa wakimbizi kutoka Nigeria waliovuka mpaka kuingia nchi hiyo jirani. Maafisa wamesema wana wasiwasi hasa kuhusu hali za wanigeria 30,000 na watoto wapatao 100 walioko katika kambi ya wakimbizi ya Minawao, ilioko wilaya ya Mayo Tsanaga, nchini Cameroon.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman,afp
Mhariri:Gakuba Daniel