1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Niger latangaza rasmi mapinduzi dhidi ya Bazoum

Grace Kabogo
27 Julai 2023

Kundi la wanajeshi wa Niger limetangaza rasmi kumuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum, masaa machache baada ya kiongozi huyo kuzuiliwa ndani ya ikulu na kikosi chake cha walinzi.

https://p.dw.com/p/4US0r
Niger | TV-Ansprache Colonel Major Amadou Adramane
Picha: ORTN/REUTERS TV

Wanajeshi hao wametoa tangazo hilo kupitia televisheni ya taifa usiku wa kuamkia Alkhamis (Julai 27) kupitia taarifa iliyosomwa na Kanali Amadou Abdramane.

Kanali huyo ameeleza kuwa vikosi vya ulinzi na usalama vimeamua kuuondoa utawala uliopo madarakani kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama, utawala mbovu na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii.

Soma zaidi: Niger yakumbwa na kitisho cha "mapinduzi ya kijeshi"

"Mipaka ya nchi imefungwa na amri ya kutotoka nje imetangazwa nchi nzima na huduma katika taasisi zote za umma zimesitishwa hadi hapo taarifa nyingine itakapotolewa," alisema Kanali Abdramane.

Marekani na Umoja wa Mataifa zimetoa wito wa Bazoum kuachiwa huru mara moja na zimelaani vikali matukio yanayoendelea nchini Niger.

Jumuiya ya kimataifa imelaani hatua za kunyakua madaraka kwa nguvu, ambazo zinadhoofisha utawala wa kidemokrasia, amani na utulivu.