1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Pakistan laukomboa uwanja wa ndege

9 Juni 2014

Jeshi nchini Pakistan limetangaza kumalizika operesheni ya kuukomboa uwanja mkubwa wa ndege mjini Karachi kutoka mikononi mwa wapiganaji wa Taliban, mkasa uliomalizika kwa zaidi ya watu 20 kuuawa.

https://p.dw.com/p/1CEon
Sehemu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jinnah, Karachi, ikiungua baada ya mashambulizi ya kigaidi.
Sehemu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jinnah, Karachi, ikiungua baada ya mashambulizi ya kigaidi.Picha: picture-alliance/dpa

Mkuu wa Kikosi Maalum cha Jeshi kifahamikacho kama Sindh Rangers, Meja Jenerali Rizwan Akhtar, amesema operesheni hiyo iliyoanza saa 5:30 usiku wa jana (8 Juni) ilimalizika saa 10:30 alfajiri ya leo, ikiwa imevishirikisha vikosi vya usalama kwenye uwanja wa ndege, polisi ya kawaida na jeshi la Pakistan, na kwamba kwa sasa uwanja huo wa ndege uko kwenye udhibiti wa jeshi.

"Magaidi kumi waliingia kwenye uwanja wa ndege kutokea maeneo mawili tafauti wakiwa kwenye makundi ya watano watano. Tangu mwanzo wa operesheni hadi sasa, wanajeshi saba wameuawa. Lakini hakuna ndege uwanjani hapo iliyoharibiwa. Uvamizi ulifanyika kwenye sehemu ya mizigo, ambako jengo lake lilitiwa moto na magaidi, na wote wakauawa hapo hapo." Amesema jenerali huyo.

Hata hivyo, hata baada ya tangazo hili la Meja Jenerali Akhtar, mwandishi wa shirika la habari la AFP aliye kwenye Uwanja wa Ndege huo wa Kimataifa wa Jinnah, ameripoti kuendelea kusikia milio ya risasi.

Uwanja huo wa ndege ni miongoni mwa maeneo yenye ulinzi mkali kabisa nchini Pakistan. Mapigano yaliripotiwa kuendelea kwa masaa kadhaa na vituo vya televisheni vilikuwa vikionesha urushianaji risasi uwanjani hapo, huku magari ya kubebea wagonjwa yakipangizana kuhamisha majeruhi na wahanga.

Miili ya watu 26 ilioneshwa kwa waandishi wa habari, wanane kati yao wakiwa walinzi wa usalama na wanne wakiwa wafanyakazi wa Shirika la Ndege la Pakistan (PIA). Miili yote ilipelekwa kwenye hospitali kuu ya Karachi, ambako majeruhi 26 pia walikuwa wakitibiwa. Awali, ndege zote zilizokuwa zituwe kwenye uwanja huo, zilielekezwa kwenye viwanja vyengine vya ndege.

Taliban yadai kuhusika

Msemaji wa kundi la Taliban nchini Pakistan, Shahidullah Shahid, amesema kundi lake ndilo lililofanya mashambulizi hayo, akidai kuwa ni kulipiza kisasi mauaji ya mkuu wa kundi hilo, Hakimullah Mehsud, aliyeuawa kwenye mashambulizi ya ndege isiyo rubani, mwezi Novemba mwaka jana.

Hali ya kawaida kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jinnah, Karachi, kabla ya mashambulizi ya tarehe 8 Juni 2014.
Hali ya kawaida kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jinnah, Karachi, kabla ya mashambulizi ya tarehe 8 Juni 2014.Picha: picture-alliance/dpa

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Shahid ameonya kuwa mashambulizi mengine zaidi yatafanyika katika siku zijazo.

Kushambuliwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jinnah katika mji mkuu wa kibiashara, Karachi, kumefanyika huku serikali ya Waziri Mkuu Nawaz Sharif ikijaribu kufanya mazungumzo na kundi la Taliban kumaliza miaka kadhaa ya mapigano.

Hata hivyo, mazungumzo hayo yamekuwa yakivunjika mara kwa mara kwa sababu ya kiwango kikubwa cha kutoaminiana baina ya pande hizo mbili.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AP/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman