1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Syria linaihujumu Miji ya Rastane na Yabrud

6 Machi 2012

Jeshi la Syria linaendelea na hujuma zake licha ya shinikizo la kimataifa huku mjumbe wa umoja wa mataifa na jumuia ya nchi za kiarabu,Kofi Annan akitarajiwa kuwasili jumamosi ijayo nchini humo .

https://p.dw.com/p/14FeJ
Jeshi la Syria laelekea katika maeneo ya karibu na DamascusPicha: picture-alliance/dpa

Sambamba na Rastane,jeshi la Bashar al Assad limeushambulia pia mji wa Yabroud katika mkoa wa Damascus na kufanya opereshini nyengine za kijeshi pia katika mkoa wa kusini wa Deraa-hayo ni kwa mujibu wa shirika la haki za binaadam la Syria linalozungumzia juu ya raia wasiopungua sita waliouliwa.

"Tunavumulia,ni suala la uhai au kifo... amesema Anas Abou Ali,afisa mmoja wa jeshi huru la Syria,lililoundwa miongoni mwa wengineo,na wanajeshi walioasi.

"Kinachotokea Rastane ni sawa na kilichotokea Baba Amr" amesema kwa upande wake Hadi Abdallah mwanaharakati wa halmashauri ya mapinduzi yenye makao yake mjini Homs.

Kofi Annan
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuia ya Nchi za Kiarabu Kofi AnnanPicha: dapd

Sauti zinapazwa kudai opereshini za kijeshi kutoka angani dhidi ya vikosi vya Bashar al Assad.Senetor John McCain wa Marekani anasema anapendelea opereshini hizo ziongozwe na Marekani lengo likiwa kutenga na kulinda eneo salama kuweza kusafirishia misaada ya kiutu na kijeshi kwa Syria."Wakati umewadia wa kufuata siasa ya aina nyengine.Assad anabidi aelewe hatoshinda" amesema Mc Cain katika hotuba yake mbele ya baraza la Senet la Marekani.

Kwa upande wa kidiplomasia mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na jumuia ya nchi za kiarabui,Kofi Annan atakwenda Damascus jumamosi ijayo,baada ya kukutana kesho na katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiarabu Nabil al Arabi mjini Cairo.

Kwa upande wake mkuu wa opereshini za kiutu za Umoja wa Mataifa Valerie Amos anapanga pia kwenda Syria kesho kujaribu kama anavyosema "kutafuta ruhusa ya kuingizwa misaada ya kiutu bila ya pingamizi."

Russlands Außenminister Sergei Lawrow in Syrien
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rashia Sergei Lawrow (kulia)apeana mkono na rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Rashia Sergei Lavrow atakwenda kwa upande wake Cairo jumamosi hii ambako atakutana na mawaziri wenzake wa kiarabu.Wakati huo balozi wa zamani wa China nchini Syria Li Huanxi anakwenda Damascus leo kwa ziara ya siku mbili.China imeshasema mabadiliko yoyote ya kisiasa nchini Syria na kwengineko yanabidi yatokane na yafikiwe na wananchi wenyewe bila ya ushawishi kutoka nje.

Pirika pirika hizo haziashirii kumrahisishia kazi Kofi Annan ambae wadadisi wa masuala ya kisiasa wanahisi warusi ndio wanaoshikilia ufunguo wa kufanikiwa jukumu lake..

Rashia imeshaelezea shaka shaka zake dhidi ya mswaada mpya wa azimio la baraza la usalama la Umoja wa ´Mataifa kuhusu Syria,unaosemekana umeandaliwa na Marekani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkhheir/Afp/Reuters/dpa

Mhariri:Abdul-Rahman Mohammed