1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Ukraine laudhibiti mji wa Slovyansk

Admin.WagnerD7 Julai 2014

Maafisa wa ngazi ya juu wa Ukraine,Urusi na shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya wametaka juhudi za dharura kuchukuliwa kufikia makubaliano ya amani Ukraine ambako ghasia zimetawala eneo la mashariki

https://p.dw.com/p/1CWrk
Picha: Getty Images

Wakikutana hapo jana kundi hilo la wajumbe wa mazungumzo ya kutafuta amani Ukraine wametilia mkazo haja ya kuongeza kasi ya kupiga hatua kwa juhudi zitakazoleta suluhu ya mzozo huo.

Kundi hilo la wajumbe ambalo linawakilisha Urusi,Ukraine na umoja wa Ulaya pia limeitisha duru nyingine ya mazungumzo kufanyika haraka iwezekanavyo bila ya kucheleweshwa ambayo yatashirikisha kila upande unaohusika katika mzozo huo.

Jumuiya ya kimataifa yataka kusita kwa mapigano

Wiki iliyopita mawaziri wa mambo ya nje wa Ukraine,Urusi,Ujerumani na Ufaransa walitaka kuwepo makubaliano mapya ya kusitisha mapigano mashariki mwa Ukraine yatayolishirikisha shirika la OSCE baada ya serikali ya Ukraine kusitisha makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano.

Mawaziri wa Mambo ya nje wa Urusi,Ukraine,Ujerumani na wa umoja wa Ulaya
Mawaziri wa Mambo ya nje wa Urusi,Ukraine,Ujerumani na wa umoja wa UlayaPicha: Clemens Bilan/AFP/Getty Images

Hayo yanakuja huku jeshi la Ukraine likipata ushindi wao mkubwa wa kwanza tangu uasi kuzuka katika eneo hilo la mashariki baada ya kuudhibiti mji wa Slovyansk kutoka mikononi mwa waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo hilo na sasa wanaripotiwa kuusogelea mji mwingine ambao ni ngome ya waasi hao wa Donetsk.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameutaja ushindi huo wa kudhibitiwa kwa Slovyansk ukurasa mpya katika mzozo huo na kuagiza kuendelea kwa operesheni za kijeshi dhidi ya waasi hao.

Bado mapambano

Waziri mpya wa ulinzi wa Ukraine Valery Haletey amesema wataendelea kupambana na waasi hao mpaka washindwe nguvu

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Valerey Haletey
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Valerey HaleteyPicha: Reuters

Jeshi la Ukraine limesema linapania kuiteka miji yote iliyo mikononi mwa waasi ukiwemo pia wa Luhansk na wataendeleza mashambulizi hadi waasi hao wasalimu amri.Miji mingine midogo ambayo jeshi hilo imeyadhibiti ni Artemovsk na Druzhkovka ambayo kwa mara nyingine tena bendera rasmi za Ukraine zilipeperushwa.

Waasi wameapa kuendeleza mapambano yao na kusema kwa sasa wanarudi nyuma ili kuwalinda raia na kupanga mikakati mipya dhidi ya serikali.Shirika la kueteta haki za binadamu la Human Rights watch limezishutumu pande zote mbili kwa kukiuka haki za kibindamu na kuonya kuwa waasi hao huenda wakaanza sasa mbinu ya utekaji nyara na kushambulia kwa mabomu ambayo yatawaua raia.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman