1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi lafurutu ada nchini Guinee Conacry

Oumilkher Hamidou29 Septemba 2009

Zaidi ya wapinzani 150 wameuliwa ,walipoandamana kupinga kiongozi wa utawala wa kijeshi asipiganie kiti cha rais

https://p.dw.com/p/JtdY
Musa Dadis Camara,mkuu wa utawala wa kijeshi wa Guine ya ConacryPicha: dpa

Jumuia ya kimataifa inalaani vitendo vya kinyama na kikatili vilivyofanywa na jeshi la Guine ya Conakry dhidi ya wafuasi wa upande wa upinzani.Duru za kuaminika zinasema watu zaidi ya 150 wameuwawa na wengine zaidi ya elfu moja kujeruhiwa.

Utawala wa kijeshi mjini Conackry unalaumiwa kwa kuchochea "mauwaji" wakati wanajeshi walipotawanya maandamano ya upande wa upinzani na kuwauwa dazeni kadhaa ya watu pamoja na kufanya visa vya kinyama kabisa ikiwa ni pamoja na kuwanajisi wakinamama.

Upande wa upinzani unazungumzia juu ya kuuliwa watu wasiopungua 150 katika matumizi hayo ya nguvu yaliyofanywa na jeshi jana dhidi ya maelfu ya wafuasi wa upande wa upinzani.Viongozi kadhaa wa upande wa upinzani walijeruhiwa na kupelekwa hospitali kwa matibabu.Baadhi yao wametoka hospitali hii leo mfano wa Mouktar Diallo ambae ni mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Vuguvugu la kidemokrasi nchini Guinee anaelezea jinsi hali ilivyokua:

"Walifyetua risasi kutoka kila pembe,waliwapiga watu pamoja na kuwabughudhi na kuwanajisi wakinamama kinyama kabisa.Na sie viongozi wa upinzani tumejeruhiwa vibaya sana na kutokana na amri ya kiongozi wa utawala wa kijeshi,wametupeleka hospitali.Cha uhakika ni kwamba watu zaidi ya mia kama si mia mbili wameuwawa."

Jeshi limeendelea kutumia nguvu hii leo pia na kumuuwa mtoto mdogo mjini Conakry ambako milio ya risasi imekua ikisikika hapa na pale na wanajeshi wakipiga doria katika maeneo muhimu ya mji mkuu huo.

Mashahidi na shirika lisilomilikiwa na sereikali wamesema wamepokea habari za kutisha kwamba wakinamama wanaoshikiliwa katika kambi za kijeshi na vituo vya polisi wamenajisiwa.

Kwa mujibu wa mashirika kadhaa ya haki za binaadam idadi ya wahanga wa hujuma hizo za jeshi inaweza kuwa kubwa zaidi.Shirikisho la kimataifa la haki za binaadam na shirika la haki za binaadam la Guinee yanawatuhumu wanajeshi kuondowa maiti majiani ili kuficha idadi halisi ya waliouliwa.

Wafuasi wa upande wa upinzani walikusanyika jana katika uwanja wa michezo kuelezea upinzani wao dhidi ya uwezekano wa kumuona kiongozi wa utawala wa kijeshi,kepteni Moussa Dadis Camara aliyeingia madarakani kwa mtutu wa bunduki miezi tisaa iliyopita,akigombea wadhifa wa rais uchaguzi utakapoitishwa mwezi January mwakani.

Mkuu wa tume ya kuepukana na mizozo-tawi la Afrika Magharibi,Richard Monceff anasema:

"Kilichotokea jana kilikua kikitarajiwa.Jeshi ambalo hata kabla ya mapinduzi halikua na nidham,limezidi kupotoka.Kuna hofu pia miongoni mwa raia mkuu wa utawala wa kijeshi asije akagombea wadhifa wa rais uchaguzi utakapoitishwa mwezi january mwakani.Baada ya miaka 25 ya tawala za kijeshi,wananchi wa Guinee wanasema wamechoshwa."

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ,Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wamelaani vikali matumizi ya nguvu na visa vya kinyama vilivyofanywa na jeshi nchini Guinee.Ufaransa imeamua kusitisha ushirikiano wake wa kijeshi pamoja na Guinee na inatathmini upya misaada yake kwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi-amesema hayo waziri wa mambo ya nchi za nje Bernard Kouchner.

Umoja wa Afrika unandaa ripoti kuhusu visa vilivyotokea Guine pamoja na uwezekano wa kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na vikwazo.Umoja wa Afrika umempa muda Camara hadi kati kati ya mwezi ujao atangaze hadharani kwamba ataheshimu ahadi aliyotoa ya kutopigania kiti cha rais uchaguzi utakapoitishwa mwakani.

Mwandishi:O.Hamidou/AFPF

Mhariri:Abdul-Rahman