1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi latakiwa kutuliza ghasia Missouri

18 Agosti 2014

Gavana wa jimbo la Missouri,Marekani ameamuru kuwekwa kwa wanajeshi katika kitongoji cha St. Louis ambacho kimekumbwa na vurugu za ubaguzi kufuatia kuuwawa na polisi kwa kijana mmoja mweusi.

https://p.dw.com/p/1CwMQ
Waandamanaji katika mji wa Ferguson (17.08.2014)wakinyosha mikono juu kuashiria kite alichofanya Michael Brown kabla ya kupigwa risasi na kuwawa na polisi.
Waandamanaji katika mji wa Ferguson (17.08.2014)wakinyosha mikono juu kuashiria kite alichofanya Michael Brown kabla ya kupigwa risasi na kuwawa na polisi.Picha: Reuters

Gavana wa jimbo la kati nchini Marekani la Missouri leo ameamuru kuwekwa kwa wanajeshi katika kitongoji cha St. Louis ambacho kimekumbwa na vurugu zilitokana na ubaguzi kwa wiki moja sasa kufuatia kuuwawa na polisi kwa kijana mmoja mweusi.

Polisi wamekabiliana na waandamanaji katika mji wa Ferguson ulioko kwenye kitongoji cha St.Louis jana usiku waliokuwa wakipinga kuuwawa kwa kijana mweusi wa kiume Michael Brown aliepigwa risasi na polisi hapo Agusti tisa bila ya yeye mwenyewe kuwa na silaha.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 18 alipigwa risasi na askari polisi veterani.Polisi imesema kijana huyo aliekuwa akitembea barabarani kwa kukiuka sheria za barabara alisimamishwa na polisi na kikazuka kitimtimu kilichopelekea kupigwa risasi. Watu walioshuhudia tukio hilo wamepinga maelezo hayo.

Gavana wa Missouri Jay Nixon amesema hapo jana usiku polisi walifyetuliwa risasi na kurushiwa mabomu ya petroli na watu hao waliokuwa wakifanya fujo ambapo maduka pia yaliporwa.

Vitendo vimekuwa vya uhalifu

Nixon amesema watu waliojiandaa na wanaozidi kuongezeka wengi wao wakitokea nje ya jamii ya jimbo hilo la Missouri wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu wa kutumia nguvu ambavyo vinahatarisha wakaazi wa Ferguson na mali zao.

Muadamanaji katika mji wa Ferguson. ( 17.08.2014)
Muadamanaji katika mji wa Ferguson. ( 17.08.2014)Picha: Reuters

Gavana huyo amesema anaungana na watu wa mji wa Ferguson na wa jimbo zima kla Missouri kulaani kwa nguvu kitendo hicho cha uhalifu kilichojumuishwa kuwafyetulia risasi polisi ,kupigwa risasi kwa raia mmoja,kurusha mabomu ya petroli,kufanya uporaji na kujaribu kuzuwiya barabara na kukivamia kituo kikuu cha polisi.

Kutokana na hali hiyo amesema amelazimika kuwataka wanajeshi ambao waliwahi kutumika kama wanajeshi wa akiba wa jeshi la Marekani katika jimbo hilo kukabiliana na uhalifu huo ili kwamba amani iweze kurudishwa tena.

Uhalifu wa kupangwa

Kapteni Ron Johnson anayeongoza kikosi cha doria cha babarara kuu katika jimbo la Missouri amesema "Yalirushwa mabomu ya petroli,kulikuwa na mashambulizui ya risasi,uporaji,vitendo vya kihuni vya uharibifu wa mali na vitendo vyengine vya matumizi ya nguvu ambavyo inaonekana dhahir kwamba havikuzuka tu kwa ghafla bali ilikuwa ni vitendo vya uhalifu uliopangwa."

Polisi wakikabiliana na waandamanaji katika mji wa Ferguson. (18.08.2014)
Polisi wakikabiliana na waandamanaji katika mji wa Ferguson. (17.08.2014)Picha: Reuters

Vurugu hizo zimekuwa zikiendelea tokea kuuwawa kwa Michael Brown kulikoongezea mvutano kati ya waakazi weusi ambao ndio walio wengi na Idara ya Polisi ya mji wa Ferguson ambayo takriban askari wake wote ni wazungu.

Kutokana na hali hiyo kikosi cha doria ya barabara kuu katika jimbo la Missouri kimepewa jukumu la kusimamia usalama katika jimbo hilo.

Hali ya hatari

Gavana Nixon awali alitangaza hali ya hatari katika mji wa Ferguson ulioko kaskazini magharibi mwa kitongoji cha Ferguson baada ya huduma muhimu za jamii kutibuliwa.

Picha ya Michael Brown akiwa pamoja na mtoto mdogo.
Picha ya Michael Brown akiwa pamoja na mtoto mdogo.Picha: Scott Olson/Getty Images

Mapambano hayo mapya na polisi yanakuja kufuatia wiki nzima ya maandamano ya kulaani kuuwawa kwa kijana huyo mweusi wa Missouri huku serikali ikizidi kuimarisha hatua zake za kukabiliana na ghasia hizo.

Hapo jana pia Mwendesha mashtaka mkuu wa serikali Eric Holder ameamuru mchunguzi mkuu wa serikali kuchunguza tena mwili wa marehemu ambapo imeelezwa kuwa alipigwa risasi mara sita zikiwemo mbili za kichwani.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa

Mhariri : Yusuf Saumu