1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi liambatane na hali halisi

25 Juni 2010

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani,Karl-Theodor zu Guttenberg alipotembelea vikosi vyake kisiwani Cyprus, alijaribu kuvifahamisha mpango wa marekebisho yanayotazamiwa kufanywa katika mfumo wa jeshi la Ujerumani Bundeswehr.

https://p.dw.com/p/O2wl
Bundesverteidigungsminister Karl-Theodor zu Guttenberg (CSU) schreibt am Freitag (11.06.2010) vor seiner Rede im Reichstag in Berlin in seine Unterlagen. Foto: Soeren Stache dpa/lbn
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg.Picha: picture-alliance/dpa

Cyprus ni kituo cha majeshi ya Ujerumani yanayoshiriki katika operesheni ya Umoja wa Mataifa UNIFIL kuzuia usafirishaji wa silaha haramu nchini Lebanon tangu mwaka 2006. Juma lililopita, Bunge la Ujerumani lilirefusha kwa mwaka mmoja, muda wa vikosi vyake kushiriki katika operesheni hiyo ya UNIFIL. Katika siku zijazo idadi ya wanajeshi wa Ujerumani watakaopelekwa katika operesheni hiyo itakuwa 300 badala ya 800 kama ilivyo hivi sasa.

Lakini wanajeshi wa Ujerumani wanaoshiriki katika operesheni "Enduring Freedom" kupiga vita ugaidi katika Pembe ya Afika,wataondoshwa eneo hilo, mwishoni mwa mwezi huu wa Juni. Hata hivyo waziri wa ulinzi amesema, vikosi vya Ujerumani vinavyoshiriki katika operesheni "Atalanta" kupiga vita uharamia katika kanda hiyo vitabakia huko huko.

Waziri Guttenberg alikuwa akizungumza alipowatembelea wanajeshi wa Ujerumani katika manowari yao iliyotia nanga katika bandari ya Limassol kisiwani Cyprus. Manowari hiyo inashirikiana na wanamaji wa kimataifa, katika operesheni ya UNIFIL,kuzuia usafirishaji haramu wa silaha nchini Lebanon. Kushiriki kwa vikosi vya Ujerumani katika operesheni hiyo kulisababisha mabishano makali nchini Ujerumani. Kapteni Martin Kübel wa manowari hiyo ya Ujerumani, amesema operesheni hiyo imefanikiwa sana. Akaeleza kuwa licha ya ukaguzi wa zaidi ya mara elfu, hadi sasa hakuna hata meli moja iliyokutikana imepakia mizigo iliyopigwa marufuku.

Nae Guttenberg, alipozungumza mbele ya wanajeshi wa operesheni hiyo aligusia mada tete.Alisema:

"Ni dhahiri kuwa jeshi linapaswa kuchukua hatua kuambatana na mikakati yake na hali halisi ya operesheni zenyewe. Na kile kinachowezekana na kinachopaswa kutekelezwa bado hakijatokea."

Akaongezea kuwa marekebisho ya jeshini hayatofanywa kwa kuzingatia tu sera za fedha bali, ile hali halisi ya operesheni za kijeshi katika siku zijazo. Mada hiyo ni tete. Hata alipokuwa ziarani Djibouti,ripoti za mipango ya kupunguza matumizi zilizusha wasiwasi miongoni mwa wanajeshi. Lakini waziri huyo wa ulinzi hana budi kupigia upatu mpango wake wa kubana matumizi. Mbali na ujumbe huo,Guttenberg alitoa wito vile vile kutambua mchango unaotolewa na wanajeshi wa Kijerumani katika operesheni za kigeni.

Mwandishi: Nehls,Thomas/ZPR

Mhariri:Miraji,Othman