1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jiji la Bonn laandaa mkutano wa kimataifa

7 Mei 2007

Mkutano wa umoja wamataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa umeanza hii leo hapa mjini Bonn nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CHl0
Jengo la Umoja wa Mataifa mjini Bonn
Jengo la Umoja wa Mataifa mjini BonnPicha: AP

Mkutano huo unalenga kuziingiza nchi kama Marekani na China katika mkataba mpya wa kupunguza utoaji wa gesi chafu.

Zaidi ya wajumbe 1000 wanaohudhuria mkutano huo wa tarehe 7 hadi tarehe 18 ya mwezi huu wa mei wanaungana pamoja kutafuta mbinu za kuruka viunzi vya kimataifa kuhusu mkakati wa kupunguza kasi ya mabadilliko ya hali ya hewa kufikia mwaka 2012 huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Mkutano huo wa Umoja wa mataifa umependekeza mikakati zaidi katika kupambana na ongezeko la joto duniani.

Wajumbe kutoka nchi 166 wanahudhuria mkutano huu wa kwanza tangu kutolewa ripoti za tahadhari kwamba uharibifu unaosababishwa na ukame, mafuriko na kupanda kina cha maji ya bahari utaongezeka.

Yvo de Boer mkuu wa kitengo cha umoja wa mataifa kinacho shughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, amesema kupunguza kiwango cha juu cha gesi chafu inayotoka viwandani ni jambo linalohitaji kushughulikiwa kwa haraka.

Bwana Boer ameelezea hayo kutoka hapa mjini Bonn na wakati huo huo amekumbusha juu ya umuhimu wa kuzingatia zile ripoti tatu za mwaka huu wa 2007 zilizotolewa na jopo la umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.

Amefahamisha kwamba nchi masikini zinahitaji kujihusisha zaidi katika mapambano haya ya mabadiliko ya hali ya hewa na kwamba nchi zinazo endelea zinahitaji pia kupata misaada ili ziweze kujumuika vyema katika mapambano haya.

Mkutano huu wa hapa mjini Bonn unalenga kupigia mbiu mkataba mpya utakao chukua mahala pa mkataba wa Kyoto.

Marekani na China ni nchi zinazo ongoza katika uharibifu wa mazingira na haziambatani na mkataba wa Kyoto.

Umoja wa Ulaya unaounga mkono mkataba huo wa Kyoto umetoa taarifa kwamba wanasayansi wa umoja wa mataifa wamewalaumu binadamu kuwa ndio chanzo cha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Mkataba huo mpya wa kupambana na ongezeko la gesi chafu duniani unatarajiwa kujadiliwa na kupitishwa katika mkutano wa mawaziri wa mazingira utakaofanyika mjini Bali nchini Indonesia mwezi Desemba mwaka huu.

Ujerumani kwa niaba ya umoja wa Ulaya imesema kuwa katika kipindi cha miaka 10 hadi 15 kutakuwepo ongezeko la gesi chafu lakini kiwango hicho kinatarajiwa kushuka kwa asilimia 50 baada ya kipindi hicho.

Pakistan imezitaka nchi za kiviwanda kupunguza utoaji wa gesi chafu na wakati huo huo kuzipa ruzuku pamoja na utalaamu nchi zinazoendelea ili ziweze kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.