1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jim Kim ni rais mpya wa Benki ya Dunia

17 Aprili 2012

Benki ya Dunia imemchagua Jim Yong Kim, daktari wa kimarekani kuwa rais wake mpya. Kuchaguliwa kwake hakukuwashangaza wengi kwa sababu wamarekani wameiongoza benki hiyo tangu ilipoundwa mwaka 1944.

https://p.dw.com/p/14f4N
Jim Yong Kim, rais mteule wa Benki ya Dunia
Jim Yong Kim, rais mteule wa Benki ya DuniaPicha: picture-alliance/dpa

Kitu kipya katika uchaguzi huu ni kwamba mgombea huyo alikuwa na upinzani kutoka mataifa yanayoendelea. Jim Yong Kim mwenye umri wa miaka 52, na mtaalamu katika sekta za afya na elimu, alimshinda Ngozi Okonjo Iweala, waziri wa fedha wa Nigeria.

Ngozi Okonjo-Iweala, mgombea kutoka Nigeria aliyesimama dhidi ya Kim
Ngozi Okonjo-Iweala, mgombea kutoka Nigeria aliyesimama dhidi ya KimPicha: dapd

Mgombea mwingine katika wadhifa huo, Jose Antonio Okampo ambaye aliwahi kuwa waziri wa fedha wa Colombia, alijiengua Ijumaa iliyopita. Akizungumzia uchaguzi wa Kim, Okampo amesema licha ya maendeleo kadhaa, bado hakukuwa na uwazi wa kutosha.

Jose Antonio Ocampo, mgombea kutoka Colombia aliejiengua
Jose Antonio Ocampo, mgombea kutoka Colombia aliejienguaPicha: AP

''Kuna mabadiliko mazuri ukilinganisha na chaguzi zilizopita, na kuna hatua ukilinganisha na uchaguzi wa rais wa IMF mwaka jana, lakini nadhani inabidi ufanyiwe tathmini, kwa sababu siamini kwamba ulikuwa wazi kiasi cha kutosha, na uamuzi ulitegemea sifa za wagombea.'' Alisema Okampo.

Dalili ya mabadiliko

Kim atachukua nafasi ya rais wa sasa wa benki ya dunia Robert Zoellick, ambaye ataondoka mwezi June baada ya kuiongoza benki hiyo kwa muhula wa miaka mitano. Hii ni mara ya kwanza kwa wadhifa huo kuwaniwa wazi wazi, na wakurugenzi wa benki ya dunia wamewasifu wagombea wengine waliojitosa katika kinyang'anyiro hicho. Tangazo lililotolewa na benki hiyo baada ya uchaguzi wa bwana Kim, lilisema kuwa kushiriki kwa wagombea hao kumenufaisha mjadala juu ya majukumu ya rais wa benki hiyo, na dira itakayoichukua mnamo siku zijazo.

Kuteuliwa kwa Kim na Rais Obama kuliwashangaza wengi
Kuteuliwa kwa Kim na Rais Obama kuliwashangaza wengiPicha: Reuters

Chaguo la kushangaza

Kuteuliwa kwa Jim Yong Kim na Rais Barack Obama kuwania wadhifa huo kwa niaba ya Marekani kuliwashangaza wengi, kwa sababu hakuwa akijulikana katiika medani za kiuchumi. Pia kuteuliwa kwake kumebadilisha utamaduni uliozoeleka wa kuwa wadhifa huo huchukuliwa na watu wenye uzoefu katika nyanja za diplomasia na mabenki. Marais 11 waliopita, wote wamarekani, walitoka katika sekta hizo.

Rais mpya mteule wa benki ya dunia alizaliwa nchini Korea Kusini, na kuhamia Marekani akiwa na umri wa miaka mitano. Ameshiriki kwa kiwango kikubwa katika kampeni dhidi ya Ukimwi na kifua kikuu katika nchi maskini, uzoefu ambao mteuzi wake, rais Barack Obama, anasema unamfanya kuwa mtu bora zaidi kuiongoza taasisi kubwa kama Benki ya Dunia.

Robert Zoellick, rais wa Benki ya Dunia anaeondoka
Robert Zoellick, rais wa Benki ya Dunia anaeondokaPicha: dapd

''Naamini kuwa hakuna mtu mwenye sifa za kuchukua wadhifa huo kuliko Dr Jim Kim. Wakati umewadia kwa mtu mwenye uzoefu katika sekta ya maendeleo, kuiongoza taasisi kubwa zaidi ya kimaendeleo ulimwenguni.'' Alisema Rais Obama.

Shirika la misaada Oxfam limesema Jim Kim ni shujaa halisi katika sekta ya maendeleo, na ni chaguo zuri kwa Benki ya Dunia. Lakini wakati huo huo, shirika hilo limesema kuwa si rahisi kusema kuwa mtu huyo alikuwa chaguo bora, kwa sababu hakukuwepo nafasi ya ushindani wa kweli, na wenye uwazi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri:Mtullya Abdu