1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jitahada za kuwajumuisha Waroma Ulaya

27 Agosti 2010

Hatua iliyochukuliwa na Ufaransa kuwafukuza Waroma imeishtusha Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.Mkuu wa masuala ya kisheria wa umoja huo, Viviane Reding amesema, lugha iliyotumiwa katika mdahalo uliozuka ni ya ubaguzi.

https://p.dw.com/p/OxVd
EU-Justizkommissarin Viviane Reding (Luxemburg). Aufnahmedatum 23.3.2010 in Brüssel, Foto: Susanne Henn.
Mkuu wa masuala ya sheria wa Umoja wa Ulaya, Viviane Reding.Picha: DW

Umoja wa Ulaya unajaribu kuboresha hali za Waroma katika nchi wanachama wa umoja huo tangu muda mrefu. Jitahada hiyo inasifiwa na shirika la kimataifa linalotetea haki za binadamu duniani Amnesty International, lakini kwa maoni ya shirika hilo,maisha ya Waroma bado hayakuwa bora barani Ulaya.

Kwa mfano, Septemba mwaka jana, polisi katika mji wa pwani wa Burgas nchini Bulgaria waliwatimua Waroma kutoka makaazi yao na wengine waliondoshwa kwa nguvu. Makaazi hayo yalikuwepo tangu zaidi ya miaka 50 iliyopita na zaidi ya familia 40 zilikuwa zikiishi huko.

Amnesty International inasema, vitendo kama hivyo vimetoa Ugiriki,Uitalia na Rumania vile vile. Hata hivyo, mkuregenzi wa Amnesty International, Nicolas Beger anaamini kuwa maendeleo yamepatikana katika hatua za kisiasa zinazochukuliwa kuwajumuisha zaidi Waroma barani Ulaya. Kwa mfano, kila mwaka hufanywa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya kujadili hali ya kundi hilo la jamii ya wachache. Anasema:

"Maendeleo yamepatikana katika Umoja wa Ulaya, na hasa mkutano uliopita kuhusu Waroma uliweka msingi mzuri.Lakini bado tunangojea vitendo. Tunachotaka kuona ni mabadiliko ya kweli katika haki za binadamu kuhusu Waroma."

Umoja wa Ulaya unasaidia miradi ya nchi wanachama inayolenga kuyafanya maisha ya Waroma kuwa bora. Kuna mfuko maalum kusaidia miradi ya aina hiyo. Kwa mfano, zaidi ya euro milioni moja zilitumiwa kufanyia ukarabati barabara,kuwajengea watoto mahala pa kuchezea na kituo cha kuwatunza watoto katika makaazi ya Waroma nchini Hungary.

Kwa maoni ya Amnesty International, elimu ni muhimu zaidi ili Waroma waweze kujumuisha katika jamii. Lakini katika nchi nyingi ,watoto wa Kiroma hawana nafasi nzuri ya kupata elimu. Mihai Surdu wa taasisi inayoshughulikia elimu ya Waroma anasema, mfumo wa elimu hasa katika nchi za Ulaya ya mashariki na Ulaya ya kusini-mashariki hautoi nafasi sawa kwa watoto wa Kiroma ambao wengi wao hushindwa mtihani wa kuingia shule, kwa sababu hawajawahi kwenda katika shule za chekechea. Bado kuna mengi ya kutekelezwa, anasema msemaji wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Mathew Newman.

"Nchi wanachama zinapaswa kushughulikia zaidi jamii za Kiroma, hasa upande wa elimu,mafunzo na huduma za afya. Huo ni wajibu wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya."

Amnesty International inasema, Waroma wengi ni raia wa nchi za Umoja wa Ulaya kwa hivyo wana haki ya kutembea kwa uhuru katika nchi hizo.

Mwandishi:Landmesser,Wolfgang/ZPR

Mhariri: