1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joachim Gauck aapishwa

Abdu Said Mtullya26 Machi 2012

Rais mpya wa Ujerumani Joachim Gauck ameapishwa rasmi mjini Berlin. Katika maoni yake mwandishi wetu Marcel Fürstenau anasema Gauck anadhamiria kuwa Rais wa wananchi. Na atafanikiwa.

https://p.dw.com/p/14QWC
Rais mpya wa Ujerumani Joachim Gauck
Rais mpya wa Ujerumani Joachim GauckPicha: dapd

Katika hotuba yake ya kwanza, Rais Gauck alianza kwa kuuliza swali jee "watoto wetu watasema nini juu ya Ujerumani." Lakini hakuna jibu la wazi, na wala halitakuwapo. Mambo ni magumu Ujerumani na katika sehemu nyingine za dunia, kiasi kwamba majawabu rahisi hayawezi kupatikana.

Katika hotuba yake Rais Gauck alizitaja dhana kadhaa ikiwa pamoja na ubinafsi, dunia ya utandawazi, jamii za wachache, Ulaya, Mashariki ya Kati na ushabiki sugu. Kwa hayo Gauck ameonyesha matumaini juu ya kuyatimiza majukumu yake kwa mwelekeo mkubwa zaidi. Amesema anawaelewa wote waliotamauka kutokana na mivutano ya kidini,kisiasa na kijamii. Wote hao wanapaswa kupewa hisia kwamba wanasikilizwa. Gauck aliwasilisha ujumbe kwa wananchi wa Ujerumani na watu wote katika nchi za nje.

Gauck anadhamiria kuzigusa nyoyo za watu kwa kauli zake juu ya maadili ya uhuru,uwajibikaji na hali ya kuaminiana. Katika hotuba yake ya kwanza Rais mpya wa Ujerumani amethibitisha kwamba atafanikiwa kuifikia shabaha hiyo. Gauck amewashauri wananchi kuitumia kumbukumbu kama chanzo cha nguvu . Gauck mwenye umri wa miaka 72 anatumai kuungwa mkono na wengi katika hayo.

Kwa njia ya busara Gauck ameweza kuzichambua tofauti za mifumo ya kijamii katika Ujerumani iliyokuwa imegawanywa kwa muda mrefu na athari ambazo bado zipo Ujerumani na kuzigeuza tofauti na athari hizo kuwa msingi wa matumaini.

Kuhusu Ujerumani ya Magharibi, Gauck havutiwi sana na muujiza wa kiuchumi kuliko na muujiza wa kidemokrasia wa miaka ya 1950 na 1960. Gauck amepongezwa hata na wahafidhina kwa mchango wake katika harakati za mwaka wa 1968 zilizoweka msingi wa mabadiliko ya kisiasa.

Pongezi za dhati alizozipata siyo tu za heshima, kutoka pande zote zinathibitisha uwezo wa Rais huyo mpya wa kuileta jamii pamoja. Msemo kwamba "sisi ndiyo umma" kutoka Ujerumani Mashariki anakotokea Joachim Gauck bado haujapoteza maana yake katika nyakati za leo. Gauck anadhamiria kufanya juhudi ili kuyatafutia msingi wa pamoja mambo yanayotofautiana. Pia ni jambo la kulitilia maanani kwamba katika hotuba yake alimsifu Rais wa hapo awali Christian Wulff. Mamilioni ya watu nchini Ujerumani wameithamini hatua hiyo. Kwa kuyapima aliyoyasema, Joachim Gauck ameonyesha kwamba atafanya kila linalopasa ili kuwa Rais wa wananchi.

Mwandishi: Fürstenau,Marcel

Tafsiri: Mtullya Abdu

Mhariri: Abdul-Rahman, Mohamed