1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa mashariki ya kati

10 Machi 2010

Marekani yalaani Israel na mipango ya kujenga makaazi ya walowezi mashariki mwa Jerusalem.

https://p.dw.com/p/MOcW
Bw. Biden(kushoto) na Waziri mkuu wa Israel,Netanyahu mjini JerusalemPicha: AP

Shutuma dhidi ya Israel kutokana na madhumuni ya kujenga makaazi 1,600 mashariki mwa mji wa Jerusalem bado zinaendelea, huku makamu wa rais wa Marekani Joe Biden akijiandaa kukutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas leo katika mji wa Ramallah kwenye Ukingo wa Magharibi.

Mapema leo Biden amefanya mazungumzo ya faragha mjini Jerusalem na aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair ambaye ni mwakilishi wa pande nne zinazoshiriki katika mchakato wa kusaka amani ya Mashariki ya Kati zikiwemo Jumuiya ya Ulaya, Marekani, Umoja wa Mataifa na Urusi.

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon wameilaani hatua ya Israel kuridhia ujenzi wa makaazi mapya kwa walowezi wa Kiyahudi, mashariki mwa Jerusalem, jambo ambalo limewakasirisha Wapalestina.

Taarifa kutoka Umoja wa Mataifa imesema kwamba katibu mkuu, Ban ki Moon amelaani hatua ya wizara ya ndani ya Israel kuamua kujenga makaazi hayo mapya, akisisitiza kwamba ni kinyume na sheria za kimataifa.

Tangazo la Israel la ujenzi mpya wa makaazi limekuja siku mbili tu baada ya Wapalestina kukubali mazungumzo ya upatanishi baada ya miezi kadhaa ya Marekani kujaribu kuyafufua na limekuja wakati wa ziara ya Biden, ambayo ni ziara rasmi ya afisa wa ngazi ya juu zaidi katika utawala wa Rais Obama nchini Israel.

Ukosoaji wa Israel ulijiri wakati ambapo bwana Biden alikuwa akinuia kukutana na viongozi wa Israel kwa mazungumzo ya amani. Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani ilisema kwamba makamu wa rais, Joe Biden alichelewa kwa saa moja unusu kwa maandalizi ya chakula cha jioni katika makao ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Biden alisema hatua ya Israel inasaliti imani inayohitajika wakati huu na inakiuka maadili ya mazungumzo aliyokuwa nayo nchini Israel.

Msemaji wa Palestina Nabil Abu Rudeina ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hatua ya Israel itasambaratisha mchakato mpya wa kuleta amani hasa ikizingatiwa kwamba Wapalestina wanaitaka mashariki mwa Jerusalem iwe mji mkuu wa nchi walioahidiwa.

Biden alisema rais Obama na yeye wanaamini hakikisho la usalama wa Israel ni amani katika mashariki ya kati na Wapalestina pamoja na Wasyria, Walebanon ambalo hatimaye litaboresha uhusiano na mataifa ya kiarabu.

Tayari waziri wa usatawi wa Israel, Isaac Herzog ameomba msamaha kwa makamu wa rais wa Marekani Joe Biden kuhusu hatua ya ujenzi wa Israel akisema ni jambo la aibu. Naye kiongozi wa sera za nje wa Jumuiya ya Ulaya, Catherine Ashton ameilaani Israel kwa kupania kujenga makaazi 1600 ya walowezi mashariki mwa mji wa Jerusalem.

Mwandishi, Peter Moss /DPA/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo