1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

John Terry apatikana bila hatia

13 Julai 2012

Nahodha wa klabu ya Chelsea John Terry ameondolewa mashitaka ya kumtolea matamshi ya kibaguzi Anton Ferdinand wakati wa mchuano wa Ligi Kuu ya Soka ya England

https://p.dw.com/p/15XZs
John Terry of Chelsea lifts up the UEFA Champions League trophy after his team's final soccer match against Bayern Munich at the Allianz Arena in Munich, May 19, 2012. REUTERS/Dylan Martinez (GERMANY - Tags: SPORT SOCCER)
Champions League Finale 2012Picha: Reuters

Kesi hiyo ilimfanya Terry kunyang'anywa unahodha wa timu ya taifa ya England na Shirikisho la Soka la England kabla ya dimba la UEFA EURO 2012 na pia kuondoka kwa kocha Fabio Capello ambaye alitofautiana na uamuzi huo.

Baada ya kuusikiza ushahidi kwa siku nne katika mahakama moja ya mjini London, Hakimu Mkuu Howard Riddle aliamua jana Ijumaa kuwa Terry hakuwa na hatia ya kumtolea matamshi ya kibaguzi mchezaji wa Queens Park Rangers Anton Ferdinand wakati wa mchuano huo wa Oktoba mwaka jana.

Terry alisisitiza kuwa alitumia tu neno baya kama kejeli ili kujibu matamshi mabaya anayodai yalitolewa na Ferdinand. Kulikuwa na vifijo nje ya mahakama kutoka kwa jamaa za familia ya Terry baada ya kusomwa hukumu hiyo.

Bayern Munich hawajawahi kushinda kombe lolote kuu katika misimu miwili iliyopita, lakini hicho hakichawazuia mashabiki wake kutonunua tiketi za mechi zote 17 za nyumbani msimu huu kazika ligi ya Bundesliga inayoanza wiki sita zijazo.

Ndani ya uwanja wa Allianz Arena wa Bayern Munich
Ndani ya uwanja wa Allianz Arena wa Bayern MunichPicha: Daniel Martinez

Klabu hiyo imesema imeuza kila tiketi ya viti vyote vya uwanja wake wa nyumbani wenye uwezo wa kuwa na mashabiki 69,000 wa Allianz Arena, ikiwa ni takribani tiketi za simu 40,000 na zile za mashabiki karibu milioni 1.1 wa mechi za nyumbani.

Bayern ambao walsihindwa na Chelsea katika fainali ya Kombe la Ligi ya Mabingwa mwezi Mei, imewashukuru mashabiki wake kwa kudhihirisha uzalendo wao.

Msisimko wa Olimpiki uko chini Uingereza

Ikiwa imesalia wiki mbili kabla ya kuanza mashindano ya michezo ya Olimpiki mjini London, Uingereza bado haijakumbwa na msisimko wa tamasha hilo, kwa mujibu wa utafiti mpya.

Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la ComRes kwa niaba ya BBC, asilimia 61 ya Waingereza walisema kuwa kwa sasa hawajasisimkwa na mashindano ya Olimpiki kuliko ilivyokuwa mwanzoni mwa mwaka.

Hata hivyo asilimia 40 yao walisema safari ya mwenge wa Olimpiki ambayo imekaribishwa na wengi nchini humo imewapa hamu kubwa ya michezo hiyo itakayoanza tarehe 27 mwezi huu wa Julai.

Utafiti huo aidha unaonyesha kuwa asilimia 55 ya Waingereza wanaamini kuwa mashindano hayo yataifaidi nchi hiyo kwa jumla, huku wingi wa asilimia 74 wakihisi kuwa mji wa London ndio utakaonufaika zaidi kutokana na tamasha hilo.

Jiji la London litawakaribisha wageni wengi wakati wa Olimpiki
Jiji la London litawakaribisha wageni wengi wakati wa OlimpikiPicha: picture-alliance/dpa/dpaweb

Bingwa wa sasa wa Olimpiki katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Mkenya Brimin Kipruto ametabiri kuwa ushindi wa Kenya katika mbio hizo unatarajiwa kuendelea katika mashindano ya Olimpiki mjini London, baada ya nchi hiyo kuanza kutawala kitengo hicho katika mwaka wa 1984.

Kikosi cha kenya kinajumuisha bingwa wa zamani wa Olimpiki na mara mbili duniani Ezekiel Kemboi, na chipukizi Abel Mutai ambaye alishinda taji la Ubingwa wa Afrika nchini Benin mwezi uliopita.

Kipruto anayeshikilia rekodi ya muda wa kasi zaidi ulimwenguni kazika mbio za kuruka viunzi na maji anasema Kemboi aliyesmhinda katika mashindano ya Olimpiki mjini Athens mwaka wa 2004, sasa yuko katika hali nzuri na atafanya vyema.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman