1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jordan yafunga mipaka baada ya shambulizi

22 Juni 2016

Jordan imefunga mipaka yake inayoingiliana na Iraq pamoja na na Syria kufuatia shambulizi la kujitoa muhanga lilosababisha wanajeshi sita wa Jordan kuuawa karibu na mpaka wa Syria.

https://p.dw.com/p/1JBLZ
Jordanien Soldaten an Grenze zu Syrien
Picha: picture-alliance/dpa/J. Nasrallah

Wanajeshi sita wa kulinda mpaka nchini Jordan wameuawa na wengine 14 kujeruhiwa, baada ya mshambuliaji mmoja kujitoa muhanga akiwa anaendesha gari lilotegwa mabomu na kuvamia kituo cha jeshi hapo jana.

Gari hilo lilokuwa limesheheni mabomu lililipuka kilomita kadhaa mbali na kambi ya wakimbizi kutoka Syria, katika eneo lisilokaliwa na watu inapokutana mipaka ya nchi za Syria, Iraq na Jordan.

Raia kadhaa wa Jordan walikusanyika katika mkesha wa kuwaomboleza wanajeshi hawo waliouawa. Suhair Abdul Hadi, ni miongoni mwa waliohudhuria mkesha huwo.

"Nchi yetu ni nchi, na si uwanja wa vita, na kundi lolote la kigaidi au chama chochote kitakachojaribu kututisha au kutushambulia kama walivyofanya katika nchi jirani hawatofanikiwa kuingia nchini Jordan. Tumeazimia kushirikiana na jeshi ambalo lipo mstari wa mbele kupambana na magaidi," amesema Suhair Abdul Hadi.

Jordanien Anschlag an der Grenze zu Syrien
Mjeruhiwa wa shambulizi la JordanPicha: Reuters/Stringer

Kwa mujibu wa afisa wa usalama aliyekataa kutajwa kwa jina, eneo hilo la jangwa kusini - mashariki mwa Jordan kulipotokea shambulio hilo ni karibu na maeneo ya wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiisilamu IS.

Hata hivyo kundi hilo halikutoa taarifa yakuhusika na shambulizi hilo, lakini Jordan ni sehemu ya muungano wa kijeshi unaongozwa na Marekani ambao unapambana na kundi la IS nchini Syria na Iraq. Hii si mara ya kwanza, taifa hilo limeshawahi kulengwa na kundi la IS siku za nyuma.

Mfalme Abdullah wa pili ameapa kulipiza kisasi baada ya kujadiliana na maafisa wa kijeshi juu ya shambulizi hilo lilotokea karibu na eneo ambapo maelfu ya wakimbizi wa Syria wamekwama.

Taarifa ya jeshi imesema mtu huyo aliyejitoa muhanga alitokea katika kambi hiyo na kuingia ndani ya mpaka wa Jordan kupitia njia ya kuingizia misaada ya kiutu, na baadae kujiripua akiwa ndani ya gari hilo alipokaribia kituo cha mpakani cha jeshi la Jordan.

Hili ni shambulizi la kwanza la aina hii kutoka Syria linaloilenga Jordan, tokea Syria ilipotumbukia katika mgogoro mwaka 2011. Kabla ya hapo Juni 6, kulitokea shamulizi dhidi ya ofisi ya usalama karibu na mji mkuu wa Jordan amman na kusababisha vifo vya watu watano, ikiwa ni pamoja na maafisa watatu wa kijasusi wa Jordan.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef