1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JUBA : Uganda na waasi waanza tena mazungumzo ya amani

27 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC6l

Uganda na waasi wa LRA wameanza tena mazungumzo ya amani hapo jana wakati mpatanishi wa Umoja wa Mataifa akiyaita mazungumzo hayo kuwa ni fursa ya ama mbivu au mbichi katika kukomesha vita katili vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 20.

Rais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano ambaye ni mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika mchakato huo wa amani na kuheshimiwa sana barani Afrika kwa umahiri wake wa kushawishi amefunguwa mazungumzo hayo katika mji mkuu wa kusini mwa Sudan wa Juba.

Chissano amekuwa mtu muhimu katika hatua za kukwamua mazungumzo hayo baada ya kusitishwa kwa miezi mitatu.

Amewaambia wajumbe wa serikali na waasi wanaohudhuria mazungumzo hayo kwamba iwapo fursa hiyo itapotea haitorudi tena.

Kuanza tena kwa mazungumzo hayo pia kumehudhuriwa na Rais wa Sudan ya kusini Salva Kiir,mpatanishi mkuu na makamo wa rais wa jimbo hilo Riek Machar na wasuluhishi wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,Kenya,Afrika Kusini, Tanzania na Zambia.