1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za amani Caucasus

Hamidou, Oumilkher12 Agosti 2008

Rais Nicholas Sarkozy aendesha juhudi za kumaliza vita katika Ossetia ya kusini

https://p.dw.com/p/Evke
Rais Mikhail Saakashvili wa georgiaPicha: AP



Urusi imeamua kuweka chini silaha katika vita dhidi ya vikosi vya Georgia katika jimbo  lililojitenga la Ossetia ya kusini.Uamuzi huo wa Moscow umesadif wakati ambapo wawakilishi wa jumuia ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya OSCE na Umoja wa Ulaya wameingia mbioni mijini Moscow na Tbilissi kuwasihi viongozi wa pande hizo mbili wakubali kuacha uhasama.


Baada ya mazungumzo kati ya mwenyekiti wa jumuia ya Usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE mjini Moscow,hivi punde ilikua zamu ya mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya ,rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy kuzungumza na kiongozi mwenzake wa Urusi Dmitri Medvedev.


Baada ya mazungumzo ya ana kwa ana kati ya marais hao wawili,waziri mkuu wa Urusi Vladimir Putin akajiunga  nao pia mazungumzoni katika  ofisi ya rais mjini Moscow.


Mwanzoni mwa mazungumzo yao,rais Nicholas Sarkozy amesifu uamuzi wa rais Dmitri Medvedev wa kusitisha opereshini za kijeshi za Urusi-uamuzi uliopitishwa kabla ya ndege ya mwenyekiti huyo wa zamu wa Umoja wa ulaya kutuwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Moscow.


"Inabidi hivi sasa makubaliano ya kuweka chini silaha yatekelezwe,panahitajika ratiba ili kuhakikisha kila upande unarejea haraka katika maeneo ya kabla ya vita" amesema hayo rais Sarkozy mbele ya waandishi habari walioruhusiwa kushiriki katika dakika za mwanzo za mazungumzo.


Mpango wa amani ulioandaliwa na Ufaransa,kama mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya,unazungumzia juu ya kusitishwa uhasama,kuwekwa kikosi cha kulinda amani cha Urusi na Georgia pamoja na kurejea wanajeshi wa pande hizi mbili katika vituo vyao vya awali.


Hapo awali waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrow aliondowa uwezekano wa kujumuishwa Georgia katika kikosi cha kimataifa cha kulinda amani.


Jana lakini rais Dmitri Medvedev aliunga mkono  fikra ya kuwepo tume ya jumuia ya Usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE,ambayo tokea hapo ina wasimamizi wake huko Georgia.



Akitangaza uamuzi wa kusitisha mapigano rais Medwedew alisema:



"Nnaamua opereshini za kijeshi zisitishwe haraka.Vikosi vyetu vimeiitia adabu Georgia na usalama wa raia zetu na wanajeshi wa kulinda amani wa Urusi katika Ossetia ya kusini umedhaminiwa.Lakini pindi vikosi vyetu vikishambuliwa,vitalipiza kisasi."


Kwa upande wake rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy amesema tunanukuu:


"Ulimwengu unaihitaji kushirikiana na Urusi katika kadhia muhimu mfano mradi wa kinuklea wa Iran,amesema rais Nicholas Sarkozy na akuendelea "Dunia inaihitaji Urusi inayobidi kutegea nguvu zake katika juhudi za amani."Mwisho wa kumnukuu.


Wakati huo huo vikosi vya kulinda amani vya Urusi vimezungumzia juu ya hujuma za hapa na pale za baadhi ya wanajeshi wa Georgia dhidi ya vituo vya Urusi huko Ossetia ya kusini.Georgia imesema imewakusanya wanajeshi wake karibu na Tbilissi ili kuuhami mji mkuu huo.


Rais Michael Saakashvili akihutubia umati wa watu hii leo

ameamua kuitoa Georgia kutoka jumuia ya mataifa huru ya zile zilizokua jamhuri za zamani za Usovieti.