1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kidiplomasia Mashariki ya Kati.

13 Aprili 2009

George Mitchell anatazamiwa kuzuru mashariki ya kati leo , hii ikiwa ni ziara yake ya tatu kwa ajili ya kuwa na mazungumzo na viongozi wa eneo hilo.

https://p.dw.com/p/HVdt
Mjumbe maalum wa Marekani, Mashariki ya Kati, George Mitchell.Picha: AP


Juhudi za kuyapa nguvu mazungumzo kati ya Palestina na Israel yanaendelezwa kila upande. Rais wa Palestina Mahmoud Abbas jana alikuwa Riyadh, kukutana na Mfalme Abdullah kujadili namna ya kushirikiana na utawala mpya wa Israel unaoongozwa na Benjamin Netanyahu.

Mitchell anatazamiwa kukutana na maafisa kutoka Israel, Palestina na Misri, katika ziara yake ya tatu mashariki ya kati tangu ateuliwe na utawala wa Obama kama mjumbe maalum.


Na kabla ya kuwasili kwa Mitchell, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa mara ya kwanza tangu kuingia madarakani aligusia kuwa yu tayari kufanya mazungumzo na Wapalestina.


Symbolbild Netanjahu und Abbas Frieden
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Taarifa kutoka ofisi ya Netanyahu imesema, Waziri mkuu huyo alizungumza kwa njia ya simu na rais wa Palestina Mahmoud Abbas. Netanyahu anasemekana alimwambia Abbas, kuwa ana hamu ya kuendeleza ushirikiano na majadiliano ya tangu zamani ili kuleta amani kati ya Israel na Palestina.


Taarifa hiyo hata hivyo haikugusia kuundwa kwa taifa la Palestina- ahadi Israel ilikuwa imetoa katika ule mkakati wa amani wa mwaka 2003- mpango Netanyahu anaupinga.


Abbas amesisitiza serikali mpya ya Israel lazima ikubali kuwekwa kwa dola mbili ya Wapalestina na Israel zitakazoishi kwa amani kabla ya kuanza upya kwa mazungumzo ya amani, msimamo unaoungwa mkono na Marekani.

Jana pia Abbas alikuwa Riyadh Saudi Arabia, kwa ziara ya siku moja kukutana na mfalme Abdullah. Duru za kidiplomasia zinasema mkutano huu ulipigia darubini namna dola za kiarabu zitakavyoshirikiana na utawala mpya wa Israel katika kusuluhisha mzozo wa jadi kati ya Palestina na Israel.


Mazungumzo baina ya Palestina na Israel yalivunjika, baada ya waziri mpya wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman kutoa matamshi ya kupuuzilia mbali makubaliano ya mwaka 2007 ya Annapolis yanayotilia mkazo juu ya suala la kuundwa kwa dola mbili.


Ujumbe wa mashariki ya kati pia utakuwa ajenda muhimu katika mkutano wa Rais Obama na mfalme wa Abdullah wa Jordan baadaye mwezi huu mjini Washington.


Mkutano huo utaangazia juhudi za kufikia lengo la kuundwa kwa dola mbili- mkakati unaosemekana utakuwa suluhu ya mzozo huu wa Palestina na Israel. Mfalme Abdullah atakuwa anawasilisha msimamo wa nchi za kiarabu kuhusiana na swala zima la mashariki ya kati.


Mwandishi Munira Mohammed/AFPE

Mhariri Saumu Mwasimba.