1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za Kidiplomasia zachachamaa Ghuba

Saumu Mwasimba
10 Julai 2017

Rex Tillerson anaelekea Kuwait nchi inayosuluhisha mgogoro wa Qatar na nchi nne za kiarabu kujaribu kutafuta ufumbuzi wa kishindo kinachoendelea

https://p.dw.com/p/2gFxc
USA Außenminister Tillerson trifft Amtskollegen Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani aus Katar
Picha: Reuters/Y. Gripas

Mgogoro kati ya Qatar na nchi nne za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia unaendelea ambapo Qatar imesema inajiandaa kuchukua hatua za kutafuta kulipwa fidia kwa hasara iliyoipata kutokana na kuwekewa vizuizi na nchi hizo. Tangazo hilo linakuja wakati ambapo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson anatarajiwa leo(10.07.2017) kuelekea Kuwait kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo ambao hauonekani dalili za kutatuliwa kwa sasa.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani anakwenda Kuwait baada ya Jumapili  kukutana mjini Istanbul na mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglu ambako walitarajiwa kujadiliana kwa kina juu ya mvutano kati ya Qatar na nchi nyingine za kiarabu sambamba na suala la Syria. Tillerson atatumia muda wa hadi Alhamisi kuendeleza juhudi za kutafuta ufumbuzi wa kitendawili cha mvutano huu ambapo pia atakwenda nchini Saudi Arabia. Ziara ya Tillerson Kuwait inakuja baada ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson naye mnamo siku ya Jumamosi kuzitolea mwito nchi za kiarabu kufikisha mwisho hatua yao ya kuigomea Qatar huku akiondowa uwezekano wa kutokea mapambano aina yoyote ya kijeshi katika mgogoro huo mbaya kabisa kuwahi kulikumba eneo la Ghuba kwa miaka. Johnson alikutana na mwenzake wa Kuwait Sheikh Sabah al-Sabah na alipangiwa vile vile siku hiyo kwenda Qatar.

Münchner Sicherheitskonferenz
Picha: REuters/M. Dalder

Ni zaidi ya mwezi mmoja tangu ulipozuka mgogoro huu wa kidiplomasia katika eneo hilo la Ghuba na matumaini ya kupatikana suluhu yanaonekana kudidimia. Pande zote mbili yaani kundi linaloongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Qatar zikijumuisha nchi za Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri zinaelekea kuimarisha misimamo yao kuliko ilivyokuwa huko mwanzo na kamwe hakuna dalili yoyote inayojitokeza kuonesha uwezekano wa kupatikana suluhu kutoka pande zote kwa wakati huu. Hata Marekani nayo imeshadokeza kwamba haioni uwezekano wa mgogoro huu kumalizika haraka.

Julai 6 msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Heather Nauert alisema wazi kwamba wanaamini kwamba ni mgogoro utakaoendelea kwa wiki nyingine kadhaa  na pengine hata miezi.Kadhalika Taarifa iliyotolewa na msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani pia imeonya kwamba kuna uwezekano mgogoro huu ukazidi makali.Jana serikali ya mjini Doha ilitangaza kwamba inaunda kamati itakayofuatilia hatua ya nchi hiyo kulipwa fidia kutokana na madhara iliyoyapata kwa kutengwa na nchi hizo nne za kiarabu.

Ägypten Außenminister Treffen in Kairo
Mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia,Umoja wa Falme za Kiarabu,Misri na Baharain walipokutana 05.07.2017Picha: Reuters/K. Elfiqi

Mwendesha mashataka mkuu wa serikali wa Qatar Ali-Al Marri amewaambia waandishi habari mjini Doha kwamba kamati inayoundwa itashughulikia madai  kuhusu hasara yaliyotolewa na makampuni binafsi,taasisi za umma na watu binafasi na sambamba na hilo kamati hiyo itatumia mifumo ya kisheria ya ndani na Kimataifa kudai fidia hiyo  na pia itashirikiana na ofisi za sheria za ng'ambo kuyafanyia kazi madai yaliyotolewa.Qatar pia inasisitiza kwamba hatua za kisheria za kudai fidia hazifungamanishwi na suala la mazungumzo kati ya Qatar na nchi hizo nne na kusisitiza kwamba kuna tafauti kati ya siasa na sheria na suala la fidia linahusu sheria.

Saudi Arabia,Umoja wa Falme za Kiarabu,Misri na Baharian zilikata uhusiano wa kidiplomasia na wa safari za anga ardhini na baharini na nchi hiyo ya Qatar ambayo ina utajiri wa gesi asili kwa kuituhumu nchi hiyo kuwa na mafungamano na makundi ya kigaidi ikiwa ni pamoja na kuyasaidia makundi ya itikadi kali.Qatar lakini inakataa kuyakubali madai hayo na zaidi ya hilo imekataa pia kuyatekeleza matakwa yaliyotolewa na nchi hizo nne.

Mwandishi-Saumu Mwasimba/ap/reuters

Mhaririri-Josephat Charo