1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kidiplomasia zashika kasi

Oumilkher Hamidou8 Januari 2009

Makundi manane ya wapalastina yanapinga mpango wa amani ulioshauriwa na Misri na Ufaransa

https://p.dw.com/p/GUYK
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy akizungumza na kiongozi mwenzake wa Misri,Mohammed Hosni Mubarak mjini CairoPicha: AP


Katika wakati ambapo juhudi za kidiplomasia zimeshika kasi,Hamas wanasema mpango wa kuweka chini silaha ulioshauriwa na Misri haufai.


Matamshi hayo ya Hamas na makundi mengine ya wapalastina yametolewa katika wakati ambapo rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa na kansela Angela Merkel wa Ujerumani wamezungumzia utayarifu wao wa kutia njiani mkakati wa pamoja kusaidia amani ya Mashariki ya kati.


Katika mkutano wao pamoja na waandishi habari,mwishoni mwa mazungumzo yao mjini Paris,rais Nicolas Sarkozy amesema tunanukuu:"silaha lazima zisite,hali itulie,Israel ipatiwe thibitisho la usalama wake na kuihama Gaza haraka iwezekanavyo.Mwisho wa kumnukuu rais Nicolas Sarkozy aliyeongeza "wako tayari kutia njiani mkakati wa pamoja kusaidia amani ya mashariki ya kati.


Hata hivyo Chama cha Hamas na makundi mengine ya Wapalastina yanayokutikana mjini Damascus, nchini Syria, yanautia ila mpango wa amani ulioshauriwa na Misri kwa ushirikiano pamoja na Ufaransa. Wanasema mpango huo hauna msingi madhubuti na umelengwa kuyadhoofisha madai ya wapalastina.


Msemaji wa chama cha ukombozi wa Palastina, PLF, Khaled Abdel-Majid, ameliambia shirika la habari la Ufaransa, makundi manane ya kipalastina yenye makao yao mjini Damascus yamepitisha uamuzi huo baada ya mashauriano yao. Makundi hayo ni pamoja na Hamas na Jihad. Itafaa kusema hapa kwamba mkuu wa Hamas, Khakled Mechaal, anaishi pia uhamishoni mjini Damascus.


Makundi hayo yanapinga pia kuwepo vikosi vya kimataifa huko Gaza. Badala yake, makundi hayo yanataka hujuma za Israel zisitishwe, vikosi vya Israel virejee nyuma haraka na vifunguliwe vivukio vya kuingia Gaza, ikiwa ni pamoja na kile cha Rafah kati ya Misri na Gaza.


Mpango ulioandaliwa na rais Hosni Mubarak, kwa ushirikiano pamoja na rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, unazungumzia pia juu ya kuwekwa chini silaha haraka na kwa muda, ili njia iweze kufunguliwa kuingiza misaada inayohitajika ya kiutu, kuendelezwa juhudi za Misri za kusaka makubaliano ya kudumu ya kuweka chini silaha na kufikiwa makubaliano ya kusimamia usalama katika mipaka ya Gaza kabla ya kufunguliwa upya.