1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kubadilisha 'Obamacare' zashindwa tena

John Juma
28 Julai 2017

Wajumbe watatu wa chama cha Republican cha Rais Donald Trump waliungana na wenzao wa chama cha Democratic kuupinga mswada huo ulionuia kuifuta bima ya afya nchini humo maarufu kama Obamacare.

https://p.dw.com/p/2hIZ9
USA Bekanntmachung vom neuen Foxconn-Fabrik in Wisconsin
Picha: picture-alliance/CNP/AdMedia/C. Kleponis

Kwa mara nyingine Rais wa Marekani Donald Trump amepata pigo dhidi ya lengo lake la kuifuta sheria ya bima ya afya iliyoanzishwa na mtangulizi wake Barrack Obama. Hii ni baada ya mswada wa marekebisho maarufu kama "Skinny bill" ulionuia kuifanyia marekebisho sheria ya Obamacare kushindwa bungeni.

Wajumbe watatu wa chama cha Republican cha Rais Donald Trump waliungana na wenzao wa chama cha Democratic kuupinga mswada huo ulionuia kuifuta bima ya afya nchini humo maarufu kama Obamacare. Katika kura iliyopigwa usiku wa kuamkia leo, upinzani ulishinda kwa jumla ya kura 51 huku waliouunga mkono mswada huo wakipata kura 49.

Seneta wa jimbo la Arizona John Maccain wa chama cha Republican amesema anataka hakikisho la hatua zinazopaswa kuchukuliwa na kwamba taratibu zote zitafuatwa, jambo alilosema kwa sasa halipo.

Seneta John McCain
Seneta John McCainPicha: Getty Images/J. Sullivan

McCain ameongeza kuwa: "Nilivyoeleza mapema wiki hii, siungi mkono mswada huu jinsi ulivyo. Ninashauriana kwa karibu na gavana wa Arizona Doug Doocey kuhusu mswada huo unaoitwa ubadilishaji kidogo hasa athari au faida zake kwa jimbo la Arizona. Wazo langu litaongozwa na tathmini yake kuhusu namna mswada huu utakavyowasaidia watu wa jimbo langu."             

Juhudi zimeshindwa mara kadhaa

Warepublican wamekuwa wakitaka bima ya afya ya Obamacare ifutiliwe mbali au ifanyiwe marekebisho, na Rais Trump amefanya angalau majaribio kadhaa katika wiki zilizopita kuifuta sheria hiyo lakini bila mafanikio. Lau mswada wa kuufanyia marekebisho ungalipitishwa, basi baadhi ya vipengee muhimu vingeondolewa kikiwemo takwa la Wamarekani kununua bima ya afya la sivyo wapigwe faini.

Seneta Chuck Schumer akiwaongoza wenzake wa Democrat kuelekea bungeni kabla ya kura
Seneta Chuck Schumer akiwaongoza wenzake wa Democrat kuelekea bungeni kabla ya kuraPicha: picture alliance/dpa/AP Photo/B. Ceneta

Kiongozi wa walio wengi bungeni Mitch McConnel ameelezea masikitiko kuwa kwa mara nyingine wameshindwa kupitisha mswada wa marekebisho au kubadilisha bima hiyo. "Bwana rais, bila shaka ni wakati wa kusikitisha. Kuanzia gharama za juu, soko kuporomoka na wananchi wetu kuteseka chini ya bima ya afya ya Obamacare, tulifikiri wanahitaji bima bora, ndiyo maana mimi na wenzangu tulifanya tulivyoahidi kujaribu kuibadilisha sheria hii iliyofeli. Lakini juhudi zetu hazijafua dafu"

Trump awalaumu maseneta

Akizungumzia kushindwa kwa mswada huo, Rais Donald Trump ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa Warepublican watatu na wanachama 48 wa chama cha Democratic wamewaangusha Wamarekani. Saa chache kabla ya kura hiyo, ofisi binafsi ya bajeti ilitoa uchambuzi wake kuwa mswada unaopendekezwa utawaacha zaidi ya Wamarekani milioni 15 bila bima katika mwaka 2018 ukilinganishwa na sheria iliyoko kwa sasa

Mwandishi: John Juma/APE/DPAE
Mhariri:Josephat Charo