1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misitu ihifadhiwe

6 Desemba 2015

Serikali za mataifa zaidi ya dazeni moja ya Afrika zimetetea umuhimu wa kuhifadhiwa misitu ya bara hilo. Ahadi hizo zimetolewa wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/1HID5
Msitu wa Bwumba wa Zambia unavyoteketezwaPicha: picture-alliance/Balance/Photoshot

Sayari ya dunia imepoteza zaidi ya nusu ya misitu yake kutokana na sababu zilizosababishwa na binaadam. Hayo ni kwa mujibu wa taasisi ya Mali asili ya kimataifa. Visa vya kufyekwa misitu katika nchi zenye misitu ya joto vimechangia katika mabadiliko ya tabianchi kwa kueneza hadi asili mia 25 ya moshi unaichafua mazingira.

Mpango uliopewa jina AFR100 ni mkakati wa mataifa ya Afrika wa kueneza hekari milioni 100 ya misitu hadi ifikapo mwaka 2030.

"Katika wakati ambapo ulimwengu ulimwengu unalenga kufikia makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi mjini Paris,mataifa ya Afrika yenye kubeba jukumu dogo kabisa miongoni mwa wale wanaohusika na uchafuzi wa mazingira-yanaonyesha kukamata mstari wa mbele wakijitokeza na mkakati mkubwa wa kueneza misitu" amesema Andrew Steer, ambae ndie mwenyekiti wa taasisi ya mali asili ulimwenguni.

Kueneza misitu ni faida kwa wakaazi wa vijijini na mijini

Wanjira Mathai,binti ya marehemu mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Wangari Maathai, ameutaja mpango wa AFR100 wa kueneza misitu kuwa hauna mfano.

Symbolbild Erde Umweltschutz Rettung
Matumaini ya kuyanusuru mazingira,mmea waoteshwa jangwaniPicha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

"Nimeona mipango ya kueneza misitu miongoni mwa jamii katika viwango vidogo mpaka vipana barani Afrika, lakini ahadi ya kueneza misitu kote barani Afrika, kusema kweli ni wa aina yake na unatia moyo", amesema Mathai,ambae ni mwenyekiti wa vuguvugu la Ukanda wa kijani-Green Belt,ulioanzishwa na marehemu mamaake, Wangari Maathai.Kutengeneza mandhari ni faida kwa jamii zote: wakaazi wa vijijini wataimarika na kuneemeka na wakaazi wa mijini pia watafaidika.

Wakati wa warsha kuhusu mandhari jumla iliyofanyika katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi unaosimamiwa na Umoja wa mataifa, benki kuu ya dunia na serikali ya Ujerumani na washirika wengine wametenga zaidi ya dala bilioni moja kugharimia miradi ya maendeleo na dala milioni 540 kama fuko la kibinafsi kugharimia miradi ya kueneza upya misitu barani Afrika.

Mataifa kadhaa ya Afrika,yakiwemo pia yale ya maziwa makuu yaelezea azma ya kueneza misitu

Mataifa zaidi ya dazeni moja ya Afrika,yakiwemo Ethiopia, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda zimetangaza mamilioni ya hekari kwaajili ya mradi huo. Mataifa ya Afrika magharibi yanayopakana na jangwa la Sahara nayo pia yametangaza mpango wa kuotesha miti zaidi ili kuzuwia kutapakaa jangwa na kuteketeza ardhi ya kilimo.

Lemuren Indri
Aina ya kima anaekutikana katika kisiwa cha Madagascar tu.Picha: imago/blickwinkel

"Kurejesha mandhari yetu kutaleta neema,usalama na kutupatia fursa mpya,amesema Vincent Biruta,ambae ni waziri wa mali asili wa Rwanda. "Kwa kuenezwa mandhari ya misitu tumeshuhudia kuongezeka mazao ya kilimo na wakulima katika maeneo ya mashambani wamezidisha mifugo yao na kuimarisha hali yao ya maisha. "Mandhari ya misitu sio mkakati wa mazingira peke yake,ni mkakati wa kiuchumi na maendeleo ya jamii pia. "Amesema waziri huyo wa mali asili wa Rwanda.

Madagascar pia ni miongoni mwa nchi zilizoahidi kueneza misitu. Katika misitu ya kisiwa hicho kikuu kunakutikana mimea adimu duniani na wanyama wa aina pekee pia-na wote hao wanakabiliwa na kitisho cha kutoweka kutokana na mitindo ya kuteketezwa misitu.

Badhi ya nchi za bonde la Congo,linalotajwa kuwa pafu la pili la dunia baada ya lile la Amazon,katika eneo la latin Amerika, zimeelezea pia utayarifu wao wa kueneza misitu. Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo imetangaza kutenga hekari milioni 8 kwaajili hiyo.

Lakini miradi hiyo inaweza kukabiliana na shinikizo la makampuni ya mbao-chanzo kikubwa cha kukatwa miti-kwa mujibu wa shirika linalopigania usafi wa mazingira Greenpeace. Licha ya kuwepo sheria zinazokataza kukatwa miti kinyume cha sheria, visa hivyo bado vinaendelea.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir(AP

Mhariri: Amina Abubakar