1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuhifadhi mazingira

Oummilkheir16 Machi 2007

Mkutano wa mawaziri wa mazingira wa nchi 8 tajiri kwa viwanda na wenzao wa nchi 5 zinazoinukia

https://p.dw.com/p/CHI1
Wanaharakati wa Greenpeace
Wanaharakati wa GreenpeacePicha: AP

Mawaziri wa mazingira wa nchi nane tajiri kwa viwanda na wenzao wa mataifa matano yanayoinukia kiuchumi,yaani China,India,Brazil,Mexico na Afrika kusini wanakutana kuanzia leo mjini Postdam,karibu na Berlin kufikiria mbinu za pamoja kupambana na shida zinazosababishwa na kuzidi ujoto ulimwenguni.

Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika katika kasri mashuhuri la CECILIENHOF mjini Postdam ,unatoa fursa ya kutafakari na kupima maoni namna yalivyo kabla ya mkutano wa kilele wa kundi la mataifa manane tajiri kwa viwanda June sita na nane ijayo mjini HEILIGENDAM-kaskazini mwa Ujerumani na kabla pia ya kuanza rasmi duru ya mazungumzo ya Bali mwezi December ujao huko Bali-kudurusu itifaki ya Kyoto itakayomalizika mwaka 2012.

Mwenyekiti wa mazungumzo hayo,waziri wa mazingira wa serikali kuu ya Ujerumani Sigmar Gabriel ,alihimiza pawepo ushirikiano wa dhati kimataifa ili kupunguza moshi wa sumu unaotoka viwandani.

“Lengo sio kufikia makubaliano hii leo , tunataka kuzungumzia wazi wazi juu ya mambo mawili,maumbile na kubadilika hali ya hewa”amesema waziri huyo wa mazingira wa serikali kuu ya Ujerumani,ambae nchi yake ndio inayoongoza kwa sasa kundi la mataifa manane tajiri kwa viwanda,linalozileta pamoja Ujerumani,Ufaransa,Italy,Uengereza,Canada,Marekani,Japan na Urusi.

“Tunataka kuzungumzia wazi wazi vizingiti vinavyozuwia kusonga mbele majadiliano ya kimataifa kuhusu hali ya hewa na namna ya kuviondowa vizingiti hivyo”-amesema waziri Sigmar Gabriel.

“Nataraji pataibuka fikra za aina mpya,mawazo mepya,na milango itafunguliwa kwasababu hiyo ndio dhamiri ya G8 na mataifa matano yanayoinukia kiuchumi” amesema kwa upande wake waziri wa mazingira wa Uengereza David Miliband.Ameelezea matumaini kuiona Marekani ambayo haijaidhinisha itifaki ya Kyoto ya kupunguza moshi wa viwandani hadi ifikapo mwaka 2012,ikibadilisha msimamo wake.

“Ama nchi zinazoinukia kiuchumi zitachagua kujiendeleza kwa kumwaga moshi mwingi wa Carbon Dioxide,na kwa namna hiyo kuyarejesa makosa yale yale yaliyofanywa na nchi za viwanda au kufuata njia ya maendeleo bila ya kuchafua mazingira” amesisitiza waziri huyo wa Uengereza.

Mwenyekiti wa Mpango wa Mazingira wa Umoja wa mataifa UNEP,Achim Steiner amesifu juhudi za China na Brazil katika kulinda maumbile na kuhifadhi halai ya hewa.

Alikua akizungumzia mpango wa jamhuri ya umma wa China wa kutia njiani nishati zinazoweza kutumika tena pamaoja na uamuzi wa Brazil kupiga marufuku kuteketezwa misitu ya Amazone.

Wanaharakati wa shirika linalopigania usafi wa mazingira Green Peace wametia nanga kwa ghafla leo asubuhi katika fukwe za ziwa Wannsee ,wakiweka mabango yenye maandishi “ G8-Acheni porojo,tunataka vitendo”.

Wanaharakati wanataka kumpa risala kila waziri anaehudhuria mkutano huo wa Postdam,wakiombwa wajiwekee lengo la kupunguza kwa asili mia 30 moshi wa gesi za sumu unaotoka viwandani hadi ifikapo mwaka 2020.

Uongozi wa idara ya kutathmini hali ya hewa nchini Marekani-National Oceanic and Atmospheric Administration NOAA umetoa ripoti inayoonyesha kua miezi ya December,January na February mwaka huu ilikua ya joto kupita wakati wowote ule tangu utafiti wa hali ya hewa ulipoanzishwa miaka 128 iliyopita.