1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuimarisha uhusiano

P.Martin5 Desemba 2008

Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari amekutana na rais mwenzake wa Afghanistan Hamid Karzai mjini Istanbul.

https://p.dw.com/p/GAOm

Mkutano huo unafadhiliwa na Uturuki katika jitahada ya kuimarisha imani na uhusiano kati ya majirani wawili.Huu ni mkutano wa pili wa kilele kufanywa kati ya Pakistan na Afghanistan katika juhudi ya kupunguza hali ya mvutano katika kanda hiyo. .

Uhusiano kati ya majirani hao wawili haukuwa rahisi,wakati Afghanistan ikiituhumu Pakistan kuwa haichukui hatua za kutosha kupambana na wanamgambo wa Kitaliban.Lakini Rais Karzai ana uhusiano wa karibu zaidi na rais mpya wa Pakistan Asif Ali Zardari.Na kumekuwepo ishara za ushirikiano kati ya majeshi ya Afghanistan,Pakistan na vikosi vya kigeni hasa kupambana na washambulizi wanaovuka mipaka.Wachambuzi wanasema,viongozi hao wawili wametambua hatari inayosababishwa na uasi wa wanamgambo kwa nchi zote mbili.

Mkutano wa leo mjini Istanbul unaongozwa na mwenyeji Rais Abdullah Gul wa Uturuki.Mkutano wa kwanza wa kille kati ya majirani hao wawili ulifanywa April mwaka 2007 kati ya Karzai na aliekuwa rais wa Pakistan wakati huo Pervez Musharraf.Kwenye mkutano huo viongozi hao wawili waliahidi kuimarisha juhudi za pamoja kupambana na wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu na wakati huo huo kuchukua hatua za kuimarisha imani.

Maeneo ya kikabila kaskazini-magharibi ya Pakistan ni ng'ome ya mamia ya wanamgambo walioikimbia Afghanistan baada ya serikali ya Taliban kung'olewa madarakani mwaka 2001 kufuatia uvamizi ulioongozwa na majeshi ya Marekani.

Pakistan inatuhumiwa na Marekani na Afghanistan kutochukua hatua za kutosha kuwazuia wanamgambo wanaovuka mpaka kushambulia majeshi ya Marekani na vikosi vya NATO kusini mwa Afghanistan.Islamabadi lakini inakanusha tuhuma hizo na imezindua operesheni za kijeshi kupambana na makundi ya wanamgambo katika eneo hilo la mpakani.Hata hivyo nchini Afghanistan wengi wana shaka iwapo Islamabad kweli itaweza kuwadhibiti baadhi ya maafisa katika idara ya upelelezi,ikisemekana kuwa wanawaunga mkono wanamgambo wa Kitaliban.

Katika miezi ya hivi karibuni,hali hiyo mbaya ya mvutano mpakani imechochewa zaidi kufuatia mashambulizi ya makombora ya Marekani yaliyolenga vituo ndani ya ardhi ya Pakistan na kuua idadi kadhaa ya watu.

Uturuki iliyo mshirika wa NATO inatumaini uhusiano wake wa kitamduni pamoja na Afghanistan na Pakistan utasaidia kuwatia moyo majirani wawili kumaliza migogoro yao na kuimarisha ushirikiano.Siku ya Alkhamisi Rais wa Marekani George W.Bush alizungumza kwa simu na Rais Gul kumshukuru kwa jitahada za Uturuki kuleta masikilizani kati ya Pakistan na Afghanistan.Uturuki imechangia wanajeshi 860 katika jeshi la kimataifa ISAF linaloongozwa na NATO kulinda amani nchini Afghanistan.Vikosi hivyo vinashirikiana na majeshi ya Afghanistan na vikosi vinavyoongozwa na Marekani kupiga vita uasi wa Taliban unaoshika kasi nchini Afghanistan.