1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kumaliza umwagaji damu nchini Syria zashika kasi

12 Machi 2012

Baadhi ya nchi za kiarabu na wanachama wa upande wa upinzani wanatoa mwito jeshi huru la Syria lipatiwe silaha .

https://p.dw.com/p/14JFI
Kofi Annan (kulia) anazungumza na rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Mjumbe wa Umoja wa mataifa na Jumuia ya nchi za kiarabu, nchini Syria, Kofi Annan, amewasili Doha-Qatar- baada ya siku mbili za mazungumzo pamoja na rais Bashar al Assad. Damu inaendelea kumwagika na upande wa upinzani umetoa mwito baraza la usalama la umoja wa mataifa likutane haraka kufuatia ripoti ya mauwaji ya wanawake na watoto wasiopungua 40 huko Homs

Mjumbe huyo wa kimataifa amepangiwa kuzungumza na viongozi kadhaa wa serikali ya Qatar kabla ya kuelekea Ankara, nchini Uturuki hii leo ambako atakuwa na mazungumzo pamoja na waziri mkuu Racep Tayyeb Erdogan.

Kabla ya kuondoka Damascus na baada ya kuzungumza mara mbili na rais Assad wa Syria, katibu mkuu huyo wa zamani wa umoja wa mataifa alisema "amepata moyo"."Hali ni mbaya na ya hatari kwa namna ambayo hakuna yeyote kati yetu sisi wawili anaeweza kuziachia juhudi hizi zishindwe."Amesema Kofi Annan.

Hata hivyo, juhudi hizo hazikuleta tija iliyokuwa ikitarajiwa. Mjumbe maalum wa kimataifa, Kofi Annan, hakupata jibu la mapendekezo aliyotowa wakati wa mazungumzo. Kofi Annan alipendekeza silaha ziwekwe chini, ipatikane njia ya kuingiza misaada ya kiutu,wafungwa waachiliwe huru na mazungumzo yaanzishwe.

Kämpfe in Syrien
Mapigano nchini SyriaPicha: picture-alliance/abaca

Juhudi za kidiplomasia zinaendelea leo pia mjini New York kati ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton, na waziri mwenzake wa Urusi Sergeui Lavrov, katika wakati ambapo baraza la usalama linasubiri kusikiliza ripoti kuhusu wimbi la mageuzi katika nchi za kiarabu.

Baraza la taifa la Syria, kundi kubwa la upinzani nchini humo, limetoa mwito baraza la usalama la umoja wa mataifa likutane haraka kufuatia ripoti za mauwaji ya halaiki ya wanawake na watoto wasiopungua 50 katika mitaa ya Karm al Zeytoun na al Adawiye huko Homs.

Na miito ya kutaka waasi wapatiwe silaha inazidi pia kuongezeka.

Mwanasiasa wa upande wa upinzani wa Syria anaeishi uhamishoni mjini Berlin, Ferhad Ahma, anasema:"Ikiwa serikali inaendelea kila siku kuuwa watu wengi kama hawa- kila siku watu wasiopungua mia moja wanauliwa nchini Syria, hapo nahisi mie, sisi ambao ndio wawakilishi wa wananchi wa Syria tunabidi tuzingatie njia nyengine, labda kulipatia silaha jeshi huru la Syria."

Syrien Freie Syrische Armee Syrien Homs
Vikosi vya jeshi huru la Syria huko HomsPicha: Reuters

Matamshi kama hayo yalitolewa hapo awali na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Saud Arabia, Saud al Faysal, na pia waziri mwenzake wa Qatar, Sheikh Hamad ben Jassem al Thani, aliyelaani "mauwaji ya halaiki ya mtindo mmoja" yanayofanywa na serikali ya Syria, akisema wakati umewadia wa kupelekwa vikosi vya nchi za kiarabu na vya kimataifa nchini Syria.

Mwandishi:Hamidou OummilkheirAFP/Reuters

Mhariri: Miraji Othman