1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuokoa maisha ya mfanyakazi

P.Martin23 Julai 2007

Mfumo wa sheria nchini Saudia Arabia unakodolewa macho na jumuiya ya kimataifa,baada ya adhabu ya kifo iliyotolewa kwa mfanyakazi wa majumbani kutoka Sri Lanka,kuahirishwa dakika ya mwisho.

https://p.dw.com/p/CB2Y

Mfanyakazi wa kigeni,Rizana Nafeek,mwenye umri wa miaka 19 alipewa adhabu ya kifo tarehe 16 mwezi Juni kwa madai kuwa kwa makusudi alimua mtoto mchanga wa miezi minne,alipokuwa akimnywesha maziwa,hapo mwezi Mei mwaka 2005.

Nafeek alipewa muda wa mwezi mmoja tu kukata rufaa au angeadhibiwa kwa kukatwa kichwa na kiwiliwili chake kuwekwa hadharani ili kuwazuia wengine kufanya kosa kama lake.

Pindi adhabu hiyo ingetekelezwa,basi ingekuwa moja miongoni mwa 100 zilizotimizwa mwaka huu peke yake.Kwa mujibu wa Amnesty International, Shirika linalotetea Haki za Binadamu Ulimwenguni, idadi ya adhabu ya kifo inaongezeka nchini Saudi Arabia.Baadhi kubwa ya watu wanaouliwa ni wageni.Saudi Arabia ina jumla ya watu milioni 27,ikiwa ni pamoja na raia wa kigeni wapatao milioni 5.5.Mwaka uliopita,nchini humo watu 39 waliuliwa baada ya kuadhibiwa kifo,na kati ya hao 26 walikuwa raia wa kigeni.

Rizana Nafeek,amesalimika chupu chupu,kufuatia juhudi za Halmashauri ya Haki za Binadamu ya Asia -AHRC iliyo na makao yake huko Hong Kong. Halmashauri hiyo ilizindua kampeni ya kimataifa kukata rufaa,baada ya kupata idhini ya Ubalozi wa Sri Lanka mjini Riyadh na kusimamia gharama zote za kuilipa kampuni ya wanasheria wa Kisaudia, kuipinga adhabu hiyo ya kifo mahakamani.

Naibu waziri wa nje wa Sri Lanka,aliefuatana na wazazi wa Nafeek kwenda Riyadh amesema,rufaa imekatwa tarehe iliyotakikana.Ujumbe wake unaokwenda Saudia Arabia unajaribu kwa njia nyingine kuyaokoa maisha ya mfanyakazi huyo, ambae adhabu yake ya kifo imeahirishwa kwa muda tu.Ujumbe huo unatazamia kukutana na wazazi wa mtoto aliefariki,kwani kuambatana na sheria ya Saudi Arabia,ni wazazi hao tu wanaoweza kumsamehe mfanyakazi huyo,jambo ambalo walikataa kufanya, adhabu hiyo ilipotolewa.

Mkasa wa juhudi za kimataifa,kujaribu kuokoa maisha ya Nafeek,huonyesha jinsi ilivyokuwa vigumu kabisa kwa raia wengine wa kigeni walioadhibiwa,kuchukua mawakili wa Saudia Arabia,hata ikiwa wanafahamu kuwa wana haki ya kufanya hivyo.

Utaratibu wa majaji wa Saudia unachunguzwa kuhusu kesi ya Nafeek.Kwa mujibu wa AHRC,inasemekana kuwa Nafeek alimuarifu jaji kwamba alipowasili Saudi Arabia,alikuwa na umri wa miaka 17 na si 23.Pasipoti na cheti chake cha kuzaliwa zimebadilishwa na shirika lililompatia kazi.

Kwa hivyo,kilipotokea kifo cha mtoto mchanga, mfanyakazi huyo alikuwa na miaka 17,hali ambayo humaanisha yeye binafsi,alikuwa mtoto.

Saudi Arabia,imetia saini Mkataba wa Kutetea Haki za Mtoto.Mkataba huo,unapiga marufuku kwa mwanachama yo yote kutoa adhabu ya kifo kwa uhalifu uliotendwa wakati wa kuwa chini ya umri wa miaka 18.

Sasa ndio haijulikani ni lini kesi ya Nafeek itafikishwa mahakamani.