1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kusitisha mapigano Ukanda wa Gaza zaendelea

Mohammed Khelef
6 Machi 2024

Juhudi za kusitisha mapigano zinaendelea, huku jeshi la Israel likiendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza kwa makombora na Umoja wa Ulaya ukipanga kufungua njia ya kuwasaidia wakaazi wa Gaza kupitia Bahari ya Mediterenia.

https://p.dw.com/p/4dEVP
Misaada ikifikishwa kwa njia ya anga kwenye Ukanda wa Gaza.
Misaada ikifikishwa kwa njia ya anga kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Amir Cohen/REUTERS

Jeshi la Israel, ambalo limeapa kuliangamiza kundi la Hamas kufuatia mashambulizi yaliyofanywa tarehe 7 Oktoba na kundi hilo kusini mwa Israel, liliendelea na kuushambulia Ukanda wa Gaza kwa mabomu na makombora siku ya Jumatano (Machi 6), huku hali ya kibinaadamu ikielezewa kuzidi kuwa mbaya.

Soma zaidi: Westerwelle akutana na Netanyahu Jerusalem

"Khan Younis inaangamizwa kichwa chini miguu juu, huku Marekani ikidai inataka kuwalinda raia. Israel imekuwa ikiharibu nyumba na barabara kwa miezi sasa huku tukisikia ahadi za uongo za usitishwaji wa haraka wa mapigano." Shaaban Abdel-Raouf, fundi umeme wa Kipalestina na baba wa watoto watano, ambaye sasa amekimbilia mji wa kusini wa Khan Younis, aliliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu.

Soma zaidi: Mapigano yasitishwa Gaza kwa saa 12

Wakaazi wa eneo hilo, ambalo nyumba zake zilijengwa kwa ufadhili wa Qatar, waliripoti kusikia miripuko usiku mzima wa kuamkia Jumatano kutoka angani na ardhini. 

Mashambulizi dhidi ya Gaza
Matokeo ya mashambulizi ya Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Al-Nuserat siku ya tarehe 5 Machi 2024.Picha: Omar Ashtawy/APA/IMAGO

Ndege za kijeshi za Israel zilishambulia pia maeneo ya kambi ya wakimbizi ya Al-Nuseirat na mji wa Deir Al-Balah katikati ya Ukanda wa Gaza, na sehemu za mji wa kusini waRafah, walisema walioshuhudia mashambulizi hayo.

Majadiliano yaendelea Kairo

Mazungumzo ya kusaka usitishaji mapigano yaliendelea mjini Kairo kati ya wenyeji Misri, wawakilishi wa Hamas na wajumbe kutoka Qatar na Marekani. Israel haikutuma wawakilishi wake kwenye duru hii ya mazungumzo.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyokuwa yanajadiliwa na yaliyoungwa mkono na mshirika mkuu wa Israel, Marekani, yaliitaka Hamas iwaachie baadhi ya mateka inaowashikilia na kuchapisha orodha ya mateka wote wengine ilionao, huku Hamas ikitaka kuachiwa kwa mamia ya wafungwa wa Kipalestina. 

Mashariki ya Kati Kibbutz.
Ndugu na jamaa ambao ndugu zao walitekwa na kundi la Hamas wakiandamana kwenye eneo Kibbutz, ambapo mateka hao walichukuliwa tarehe 7 Oktoba 2023.Picha: Leo Correa/AP/dpa/picture alliance

Soma zaidi: Israel yaitwanga Gaza kabla ya kura ya usitishaji vita UM

Siku ya Jumanne (Machi 5), Marekani iliyapitia upya maneno kwenye rasimu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuunga mkono kile inachokiita "usitishwaji wa haraka wa mapigano kwa takribani wiki sita kwenye Ukanda wa Gaza pamoja na kuachiliwa kwa mateka wote", kwa mujibu wa waraka ulioshuhudiwa na Reuters.

Ulaya yataka kuwasaidia Wapalestina kupitia Mediterenia

Kwa upande mwengine, Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, alitazamiwa kusafiri kwenda nchini Cyprus wiki hii kuangalia uwezekano wa Umoja wa Ulaya kutayarisha njia salama kuwasaidia wakaazi wa Gaza kupitia Bahari ya Mediterenia.

Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen.
Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen.Picha: Yves Herman/REUTERS

"Juhudi zetu zimejikita kwenye kuhakikisha kwamba tunaweza kutowa misaada kwa Wapalestina. Tunatazamia kwamba kufungulia kwa njia hiyo kutafanyika hivi karibuni." Msemaji wake aliwaambia waandishi wa habari mjini Brussels siku ya Jumatano.

Soma zaidi: Blinken amaliza ziara ya Mashariki ya Kati baada ya Israel kukataa pendekezo la kusitisha vita

Umoja wa Ulaya umegawika baina ya mataifa wanachama yaliyo waungaji mkono wakubwa wa operesheni ya Israel katika Ukanda wa Gaza, ambapo baadhi yao yalijiunga na hatua ya kulikatia misaada Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) wakati huu vita vikiendelea; na yale ambayo yamekuwa yakiikosowa operesheni hiyo.

Vyanzo: Reuters, AFP