1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa jumuia ya Afrika Mashariki Bujumbura

6 Mei 2015

Serikali ya Burundi na upande wa upinzani wanakutana kwa lengo la kumaliza mvutano baada ya siku kadhaa za maandamano ya umwagaji damu yaliyosababishwa na azma ya rais Pierre Nkurunziza kugombea mhula wa tatu.

https://p.dw.com/p/1FKoW
Machafuko Kati ya polisi na waandamanaji mjini BujumburaPicha: picture-alliance/AP Photo//J. Delay

Shinikizo la kimataifa ndio lililopelekea kuitishwa mkutano huo .

"Huu ni mkutano wa fursa ya mwisho,wanabidi wafikie ufumbuzi thabiti kwa namna ambayo uchaguzi utaitishwa katika hali itakayokubalika kwa pande zote-amesema mwanadiplomasia mmoja aliyeonya msaada wa fedha wa kimataifa kugharimia uchaguzi huo utasitishwa pindi makubaliano yakishindwa kufikiwa.

Duru za serikali,ambazo hazikupendelea kutajwa jina sawa na mwanadiplomasia huyo,zimethibitisha kwamba serikali imekubali kuzungumza na baadhi ya washirika wa mashirika ya huduma za jamii na upande wa upinzani ili kusaka ufumbuzi.

Wawakilishi wa pande hizo zinazohasmiana nchini Burundi wameanza kukutana tangu jana usiku na mazungumzo yao yamepangwa kuendelea hii leo.

Hofu kama makubaliano yanaweza kupatikana

Mmojawapo wa viongozi wa wanaharakati wanaopinga mhula wa tatu kwa rais Nkurunziza,aliyeshiriki katika kikao cha jana cha mazungumzo ameelezea shaka shaka zake kuhusiana na matokeo ya mkutano huo akihoji serikali inapinga kuzungumza kiini cha mzozo wenyewe ambacho anasema ni mhula wa tatu.

Burundi Präsident Pierre Nkurunziza bewirbt sich um eine dritte Amtszeit
Rais anaetaka kugombea mhula wa tatu Pierre NkurunzizaPicha: Reuters/T. Mukoya

"Tumezungumza hadi usiku wa manane-amesema na kuongeza,tunanukuu" nnahofu kama tutasikilizana kwasababu serikali haitaki kuzungumzia mhula wa tatu wa Nkurunziza-lakini suala hilo ndilo lenyewe hasa kwetu sisi-haliepukiki."

Wakati huo huo ujumbe wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje kutoka Kenya,Rwanda,Uganda na Tanzania,nchi wanachama pamoja na Burundi wa jumuia ya nchi za Afrika Mashariki wamewasili Bujumbura kusaidia kuufumbua mzozo wa kisiasa unaoikumba nchi hiyo.

"Wanakuja kuzisikiliza pande zote zinazohusika na ugonvi huo na kujaribu kupendekeza namna ya kuupatia ufumbuzi" amefafanua msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Burundi Daniel Kabuto.

Hali ni tete katika baadhi ya mitaa ya Bujumbura

Mjini Bujumbura kwenyewe maripota wa shirika la habari la Ufaransa AFP wanasema polisi wanapiga doria na dazeni kadhaa ya waandamanaji wakiongozana kimya kimya katika mitaa kadhaa ya mji huo. Hata hivyo mashahidi wanazungumzia kuhusu hali inayotisha katika mtaa wa Kanyosha kusini ya mji mkuu Bujumbura kati ya waandamanaji na vijana wa chama tawala.

Burundische Flüchtlinge in Ruanda
Waburundi walioyahama maskani yao na kukimbilia RwandaPicha: S. Aglietti/AFP/Getty Images

Burundi inapanga kuitisha uchaguzi wa bunge May 26 na ule wa rais juni 26.

Wiki iliyopita jumuia ya nchi za Afrika Mashariki ilizisihi pande zinazohusika zikubali kujadiliana ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa njia huru na salama.Jumuia ya Afrika Mashariki ikaitolea wito pia Burundi ihakikishe uchaguzi huo haugeuki chanzo cha mzozo wa kijamii,ikikumbusha maelfu ya waburundi wameshaanza kukimbilia katika nchi jirani kwa hofu za kutokea machafuko wakati wa uchaguzi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga