1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaahidi kusaaidia

26 Novemba 2015

Rais wa Ufaransa Francois Hollande anakwenda Moscow kwa mazungumzo pamoja na rais wa Urusi,Vladimir Putin kujaribu kusaka msimamo wa pamoja katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislam-IS.

https://p.dw.com/p/1HCp8
Rais Francois Hollande na kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: Reuters/P. Wojazer

Rais wa Ufaransa Francois Hollande anakwenda Moscow baadae hii leo kwa mazungumzo pamoja na rais wa Urusi,Vladimir Putin.Lengo ni kujaribu kusaka msimamo wa pamoja kati ya Marekani na Urusi kuhusu Syria na pia katika mapambano dhidi ya kundi la wanamgambo wa itikadi kali wa dola la kiislam-IS.

Akiendelea na juhudi za wiki nzima za kidiplomasia ,rais Francois Hollande amekutana leo asubuhi katika kasri la Elysée na waziri mkuu wa Italy Matteo Renzi,baada ya kuzungumza jana na kansela wa Ujerumani Angela Merkel na kabla ya hapo na rais Barack Obama wa Marekani na pia waziri mkuu wa Uengereza David Cameron ambae leo hii anapanga kuwasilisha bungeni mjini London mpango kuhusu kushiriki nchi yake katika mapambano dhidi ya IS nchini Syria.

"Tunabidi tuwavunje nguvu IS kule kule mashinani nchini Syria na Irak na lengo ni kuwateketeza kabisa."Amesema rais Hollande alipomuomba kansela Angela Merkel , Ujerumani- mshirika mkubwa wa Ufaransa barani Ulaya ishiriki kuwapiga vita wanamgambo hao.Kansela Merkel alisema:"Ugaidi ni adui yetu wa pamoja.Ni jukumu letu kwa pamoja kuwapiga vita.IS hawawezi kutanabahishwa kwa maneno,wanabidi waandamwe kwa njia zote zilizopo za kijeshi."

Kansela Angela Merkel amemwaahidi Francois Hollande,nchi yake itawajibika haraka na bega kwa bega na Ufaransa katika mapambano dhidi ya IS.

Mataifa yote 28 ya Umoja wa Ulaya yako tayari kusaidia

Ujerumani ambayo haimo katika opereshini za nchi shirika nchini Iraq na Syria,imetangaza azma ya kutuma wanajeshi 650 ziada nchini Mali ili kuipunguzia mzigo Ufaransa inayopigana dhidi ya wanaamgambo wa itikadi kali tangu katika eneo la Sahel mpaka mashariki ya kati.

Bundeswehr in Mali Logo der Trainingsmission
Nembu ya jeshi la Ujerumani linalotoa mafunzo ya kijeshi nchini MaliPicha: picture-alliance/dpa/P. Steffen

Washirika wa Ufaransa katika Umoja wa ulaya wameahidi kusaidia opereshini za kijeshi za Ufaransa nchi za nje, naiwe kwa njia ya moja kwa moja au nyengineyo.habari hizo zimetangazwa na waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian bila ya kutoa ufafanuzi.

Jana usiku bunge la Ufaransa limepiga kura kwa wingi mkubwa kuruhusu nchi yao iendelee na hujuma za angani nchini Syria."Hakuna njia mbadala tunabidi tuwateketeze IS." amesema waziri mkuu Manuel Valls.

Matumaini ya kumtanabahisha Putin kujiunga na ushirika

Baada ya kufanikiwa kuishawishi Marekani iunge mkono mpango wa kuzidishwa makali hujuma za angani nchini Syria,rais Francois Hollande anatarajiwa kuwasili Moscow leo jioni kwa mazungumzo pamoja na kiongozi mwenzake wa Urusi Vladimir Putin.

Frankreich Flugzeugträger Charles de Gaulle Einsatz Syrien IS
Manuari ya kijeshi ya Ufaransa Charles de Gaule yenye kubeba ndege za kivita imeshatia nanga mashariki ya bahari ya MeditereniaPicha: Getty Images/AFP/A. C. Poujoulat

Hadi wakati huu Urusi,iliyokuwa nchi ya mwanzo kudai paundwe ushirika wa kimataifa dhidi ya wanajihadi wa IS,inacheza karata zake katika eneo hilo kwa njia moja au nyengine pamoja na Iran.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba