1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bill Clinton awasili Korea ya kaskazinni.

Abdu Said Mtullya4 Agosti 2009

Bill Clinton afanya ziara nchini Korea ya Kaskazini yenye lengo la kuwatoa jela waandishi habari wa Marekani.

https://p.dw.com/p/J3J2
Aliekuwa rais wa Marekani Bill Clinton ameanza ziara nchini Korea ya Kaskazini.Picha: AP

Aliekuwa rais wa Marekani Bill Clinton amewasili Korea ya Kaskazini katika juhudi zenye lengo la kuwezesha kuachiwa kwa waandishi habari wawili wa Marekani.Jee atafanikiwa?

Rais huyo wa zamani amewasili ghafla mjini Pyongyang ili kuongeza uzito katika juhudi zenye lengo la kuwezesha kuachiwa kwa waandishi habari wawili wa Marekani wanaotumikia adhabu ya kifungo.

Waandishi hao Laura Ling na Euna Lee walikamatwa tarehe 17 mwezi machi walipokuwa wanaripoti juu ya wakimbizi wa Korea ya Kaskazini waliokuwa wanaikimbia nchi yao.Mahakama ya Korea ya Kaskazini iliwatia hatiani wamarekani hao kwa kosa la kuvuka mpaka kinyume na sheria na kwa makosa mengine.Wanatumikia adhabu ya kifungo cha miaka 12 jela na kazi ngumu.

Ziara ya rais huyo wa zamani wa Marekani Clinton ni ya kwanza kufanywa na Mmarekani wa hadhi ya juu katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. Mnamo mwaka 1994 aliekuwa rais mwengine wa Marekani Jimmy Carter pia alifanya ziara nchini Korea ya Kaskazini.

Afisa mmoja wa wizara ya mambo ya nje amesema lengo la ziara ya Clinton ni kuwarudisha nyumbani waandishi habari hao wawili ambao wote ni wanawake.

Wachunguzi na wanasiasa wanaamini kwamba waandishi hao hatimaye wataachiwa.Wachunguzi nchini Korea ya Kusini wamesema Katika ziara yake nchini Korea ya Kaskazini bwana Bill Clinton anatarajiwa kukutana na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Il. Wachunguzi hao wamesema ziara hiyo pia inaweza kuufanya uhusiano baina ya Marekani na Korea ya Kaskazini uwe mzuri.

Uhusiano baina ya nchi hiyo ya kikomunisti na Marekani umeendelea kuwa wa mvutano kutokana na mipango yake ya nyuklia. Korea ya Kaskazini hivi karibuni ilifanya majaribio kadhaa ya silaha za nyuklia licha ya jumuiya ya kimataifa kuitaka nchi hiyo kutofanya hivyo.

Ziara ya bwana Clinton pia itaweka msingi wa mazungumzo juu ya masuala kadhaa ikiwa pamoja na juu ya mpango wa nyuklia wa Korea ya Kaskazini.

Mwandishi/Mtullya A.

Mhariri/.Agencies.

Mhariri:Abdul-Rahman