1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi zaidi kupambana na Al Shabaab zahitajika

MjahidA16 Februari 2012

Kundi la Kimataifa linaloshughulikia migogoro linasema ni lazima Kenya itafute mikakati maalum ya kushirikiana na Jamii ya Kimataifa katika kupambana na kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1442n
Jeshi la Kenya
Jeshi la KenyaPicha: dapd

Abdillahi Boru Halakhe mchambuzi katika eneo la Pembe ya Afrika akiangalia pia Kenya na Somalia, amesema iwapo Kenya itataka kufanikiwa katika vita vyake dhidi ya Al shabaab ni muhimu serikali ya nchi hiyo itafute  juhudi za kuungana na jamii ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, Marekani Uingereza na wengine kulitokomeza kundi hilo.

Abdillahi amesema tangu Kenya ilipoingia Kusini mwa Somalia Octoba mwaka jana katika oparesheni yake ya Linda Nchi na licha ya jeshi hilo kutoa taarifa za mara kwa mara kwamba limefanikiwa kudhibiti miji kadhaa nchini Somalia na kuuwa baadhi ya wanachama wa Al shabaab, bado uwezekano wa kushambuliwa vibaya na kundi hilo upo.

Mchambuzi huyo ameongezea kwamba kundi hilo huenda pia likapanga mashambulizi zaidi nchini Kenya katika kulipiza kisasi. Shirika hilo limesema jeshi la Kenya lilifanya haraka kuingia Somalia kupambana na kundi la Al Shabaab bila ya kuzingatia madhara yake.

Mpiganaji wa kundi la Al Shabaab
Mpiganaji wa kundi la Al ShabaabPicha: AP

Awali kundi la kigaidi la Al Qaida lilitangaza wazi kwamba limeungana na kundi  la Al shaabab, jambo ambalo Abdillahi anasema huenda likalipa  nguvu kundi hilo katika kutekeleza maafa zaidi na pia kujihami kisilaha na kifedha.

Kiongozi wa Al Shabaab Ahmed Godane alinukuliwa na chombo kimoja cha habari akisema ndugu zao yaani al Qaeeda wamekuwa wakishirikiana nao tangu mwaka wa 93 kutekeleza mapigano na mashambulizi kwa pamoja.

Hata hivyo  Waziri mkuu wa Somalia Abdiwali Mohamed Ali amesema tangu kitambo kundi hilo lilikuwa halifanyikazi kwa ajili ya maslahi ya wasomali lakini wamekuwa wakitekeleza wito waliokuwa wanapewa na kundi hilo.

Sasa Serikali ya Kenya itabidi ijifunge kibwebwe na kuja na mbinu kali zaidi za kupambana na kundi la Al shabaab ambalo nguvu zake huenda zikaimarika kufuatia kujiunga na kundi la Al Qaeda.

Mwandishi Amina Abubakar

Mhariri Yusuf Saumu