1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Jumapili Kabambe" ya uchaguzi wa majimbo Ujerumani

13 Machi 2016

Wajerumani Jumapili (13.03.2016) wanapiga kura katika uchaguzi muhimu wa majimbo ambao unaonekana kuwa mtihani mkubwa wa kuungwa mkono kwa sera za wakimbizi za Kansela Angela Merkel.

https://p.dw.com/p/1ICM1
Mpiga kura katika jimbo la Rheinland-Pfalz. (13.03.2016)
Mpiga kura katika jimbo la Rheinland-Pfalz. (13.03.2016)Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Wasiwasi wa wapiga kura kuhusu wimbi kubwa la wahamiaji kuwahi kushuhudiwa nchini yumkini ukakinufaisha chama cha sera kali za mrengo wa kulia cha AfD.Vituo vya kupigia kura huko Baden- Württemberg,Rhineland-Oalatinate na Saxony-Anhalt vimefunguliwa saa mbili asubuhi ambapo Wajerumani milioni 13 wanastahiki kupiga kura katika uchaguzi huo kuchaguwa wabunge ya majimbo hayo matatu.

Kile kinachojulikana kama "Jumapili Kabambe" kwa kiasi kikubwa kinachukuliwa kuwa kama kura ya maoni kwa sera ya milango wazi ya Kansela Angela Merkel kwa wakimbizi ambayo imeshuhudia zaidi ya watu milioni moja wengi wao wakiwa ni Wasyria wakiwasili nchini Ujerumani mwaka jana.

Sera yake hiyo imekuja kugawa wananchi na pia kusababisha mgawanyiko ndani ya chama cha Merkel cha CDU .Kansela huyo amekataa hatua za kuweka kikomo kwa wakimbizi wapya wanaowasili nchini na badala yake kutaka kuwagawa wakimbizi hao miongoni mwa mataifa wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya.

Merkel atetea sera ya wahamiaji

Katika mkesha wa uchaguzi huu Merkel ametetea msimamo wake huo katika mkutano wa hadhara katika mji wa Haigerloch ulioko kwenye jimbo la Baden- Wüttermberg. Amesisitiza haja ya kupunguza idadi ya wakimbizi na kuongeza kwamba wakimbizi wapya wanaowasili nchini wana wajibu wa kujijumuisha wenyewe katika jamii ya Ujerumani.

Kansela Angela Merkel katika kampeni za mwisho Baden-Württemberg 13.03.2016.
Kansela Angela Merkel katika kampeni za mwisho Baden-Württemberg 13.03.2016.Picha: picture-alliance/dpa/D. Maurer

Merkel amesema "Tunataraji wakimbizi wakubali kujumuika. Huu nji wajibu na sio chaguo"

Kushindwa kupata ushindi wa angalau majimbo mawili kati ya hayo matatu katika uchaguzi huu wa Jumapili litakuwa pigo kubwa kwa Merkel ambaye anajaribu kutaka kuungwa mkono na viongozi wa Ulaya wafikie makubaliano na Uturuki kupunguza wimbi la wakimbizi wanaoingia Ulaya.

Uchunguzi wa maoni uliofanyika awali unadokeza chama cha CDU na washirika wake katika serikali ya mseto (SPD) yumkini wakapata pigo kwa jumla wakati chama cha sera kali za mrengo wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani AfD kinatarajiwa kujipatia viti katika mabunge ya majimbo yote matatu.

CDU mashakani ?

Katika ngome yake ya jadi kusini magharibi mwa jimbo la Baden- Wüttemberg chama cha CDU kinaonekana kitapoteza kwa chama cha Kijani,kuungwa mkono kwa chama hicho kuko katika asilimia 10 hadi 29.Wakati AfD inaungwa mkono kwa asilimia 11.

Guido Wolf mgombea mkuu wa chama cha CDU Baden-Württemberg - 12.03.2016 .
Guido Wolf mgombea mkuu wa chama cha CDU Baden-Württemberg - 12.03.2016 .Picha: picture-alliance/dpa/D. Maurer

Guido Wolf mgombea mkuu wa chama cha CDU huko kusini magharibi mwa jimbo hilo anasema kampeni ya uchaguzi ya mwaka huu ilikuwa ngumu sana ambayo chama ilibidi ifanye.

Katika jimbo la Rhineland-Palatinate chama cha Merkel kinachuana vikali na chama cha SPD.Mashariki mwa jimbo la Saxony-Anhalt chama cha CDU kinaendelea kuongoza kwa kiwango kikubwa lakini AfD pia imepiga hatua hapo kwa kuwa na asilimia 18.

Kupinga wahamiaji

Chama hicho cha sera kali za mrengo wa kulia cha AfD kimefanya kampeni yake kwa kutumia ilani ya kupinga wakimbizi na imekuwa ikijaribu kuzowa kura kutoka watu waliovunjika moyo na msimamo wa serikali ya Merkel kwa wakimbizi.Katika matamshi ambayo yalizusha shutuma za kimataifa kiongozi wa chama hicho Frauke Petry alidokeza mapema mwaka huu kwamba polisi walikuwa wanapaswa kuwafyatulia risasi wakimbizi kama hatua ya mwisho kuwazuwiya wahamiaji wasiosajiliwa kuingia nchini.

Chama cha sera kali za mrengo wa kulia AfD.
Chama cha sera kali za mrengo wa kulia AfD.Picha: picture-alliance/dpa/J. Wolf

Wakati huo huo waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maziere amewatahadharisha wapiga kuzra dhidi ya kukiunga mkono chama cha AfD kwa kusema kwamba wito wake wa kufunga mipaka "unaidhuru nchi yetu."

Ameliambia gazeti la "Die Welt" chama hicho cha AfD hakina dhana ya kisiasa wala ufanisi katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya Ujerumani.

Iwapo chama hicho cha AfD kitafanya vizuri kama uchungizi wa maoni unavyodokeza washirika wa serikali ya mseto yumkini wakahitaji kushirikiana na chama chengine cha tatu ili kuweza kuwa na wingi wa viti bungeni.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP/dpa

Mhariri : Sudi Mnette