1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuia ya Ulaya EU inaendeleza jitihada zake za kuzikwamua nchi za ACP

Christopher Buke5 Novemba 2006

Taasisi ya AZISE Tanzania yaanzishwa

https://p.dw.com/p/CHLG

Jumuia ya Umoja wa Ulaya EU inatiwa moyo na Juhudi zinazoonyeshwa na viongozi wapya wa Afrika katika kupambana na Rushwa, utawala unaojali haki za binadamu na dhamira inayoonyeshwa na viongozi hao katika kuleta maendeleo katika nchi zao.

Taarifa hii inapatikana kwenye machapisho ya Umoja huo yaliyozinduliwa October 31, 2006 mjini Bagamoyo wakati wa mkutano uliozikutanisha asasi zisizokuwa za kiseriki nchini Tanzania.

EU inasema juhudi hizi zinazoonyeshwa na viongozi hawa lazima zichochewe na Jumuia hiyo ili kuhakikisha linafikiwa lengo lililokusudiwa ambalo limeainishwa kwenye mkataba baina ya Jumuia ya Ulaya na nchi za Afrika Karibian na Pacific ACP, ujulikanao kama mkataba wa COTONOU.

Kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba huo nchi wanachama zinapaswa kuhakikisha asasi zisizokuwa za kiserikali zinaundwa au kuimarisha ili zishirikishwe kikamilifu katika mchakato wa maendeleo katika nchi hizo.

Ili kufanikisha azma hii EU imekwenda umbali wa kutoa fungu maalum ili kuwezesha uundwaji na uimarishaji wa taasisi hizi.

Nchini Tanzania EU imetoa jumla ya Euro milioni 3 ambazo ni sana na shilingi bilioni 4 pesa za kitanzania kwa ajiri ya kuzijengea uwezo taasisi hizi nchini.

Msaada huu ulisainiwa November 1, 2006 mjini Bagamoyo baina ya serikali ya Tanzania na Ujumbe wa Kamisheni ya Ulaya hapa Tanzania.

Akizungumza wakati wa kusainiwa mkataba wa msaada huo Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Balozi Frans Baan alisema hiyo ilikuwa ni hatua nzuri na kusisitiza kwa lugha ya Kiswahili “ tutaendelea safari yetu kwa pamoja”, akimaanisha safari ya ushirikiano baina ya EU na ACP.

Mkutano huu kwa hiyo uliwaleta kwa pamoja Asasi zisizokuwa za kiserikali kutoka pande zote Tanzania ili kwa pamoja zipitie na kuweka mkakati wa namna ya kujiimarisha na kuwa na chombo kitakachokuwa kama jukwaa la pamoja la kukosoa, kupendekeza na kuzungumza na serikali.

Hii ni hatua muhimu kufikia vipengere muhimu vya Mkataba wa COTONOU ambavyo vina ainisha jinsi Jumuia ya nchi za Ulaya na kundi la ACP zitakavyoshirikiana katika nyanja za maendeleo, biashara, siasa, kupiga vita umaskini, kuinua demokrasia, kukuza uchumi na kujenga maendeleo endelevu.

Licha ya kuwa asasi hizi zipo katika kila nchi lakini ilikuja kubainika kuwa katika nchi za ACP hazina uwezo wa kukaa na serikali, kuangalia kukosoa na kushiriki katika mipango ya kimaendeleo inayoandaliwa na serikali zao.

Kwa hapa Tanzania jitihada za kuunda taasisi ya aina hii zilianza mapema mwezi February 2005 baada ya EU, Serikali ya Tanzania na asasi mbalimbali kukutana katika hoteli ya Kunduchi jijini Dar es salaam na kubuni aina ya muundo wa taasisi moja itakayozijumuisha asasi na taasisi zote zisizokuwa za kiserikali nchini Tanzania.

Mkutano huo uliteua Kikosi Maalum task force na kukikabidhi jukumu la kubuni na kutayarisha mpango utakaowezesha kuunda taasisi ya aina hiyo.

Kikosi hiki kilikamilisha kazi yake mwishoni mwa mwezi October baada ya mkutano huo wa Bagamoyo ambao umehitimisha kazi ya kuunda taasisi hiyo ambayo sasa inaitwa AZISE-Tanzania(Asasi Zisizokuwa za kiserikali Tanzania).

Kiasi hiki cha Euro milioni 3 kilichotolewa na EU kinakusudia kuijengea uwezo AZISE-Tanzania ifikie madhumuni yaliyokusudiwa ambayo ni pamoja na kuyajengea uwezo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, taasisi zisozokuwa za kiserikali na Jumuia za wafanyakazi.

Lengo kuu ni kufikia masharti yanayopaswa kutimzwa na nchi za ACP kuelekea Mkataba wa Cotonou na Kutoa mwongozo kuhusu mazingira yatakayowezesha asasi hizo zishiriki kikamilifu katika shughuli za ushirikiano baina ya kundi la ACP na Jumuiya ya Ulaya.

Lakini pia mchakato huu unatazamiwa kwenda umbali wa kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi wa kawaida katika mchakato wa maendeleo na masuala yenye mtizamo na mstakabali wa kitaifa.

Kwa mantiki hiyo AZISE-Tanzania ina wajibu wa kuendesha mijadala kuanzia ngazi mbalimbali za vijijini mikoani na ngazi ya Taifa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mawasiliano na mfumo wa habari utakao wezesha na kuimarisha ushirikano baina ya AZISE-Tanzania na mitandao mingine.

Wajibu mwingine wa AZISE-Tanzania ni kushiriki katika utekelezaji wa mipango na usimamizi wa miradi inayofadhiliwa na tume ya nchi za ulaya lakini hata mikataba mbalimbali ambayo Tanzania inaingia na mataifa na makampuni mbalibali.

Pia inatajwa kuwa Taasisi hii itakuwa ikikaa pamoja katika mkutano wa pembe tatu yaani AZISE-Tanzania, Jumuia ya nchi za Ulaya na Serikali ili kuangalia miradi inayoweza kuinufaisha Tanzania hususan misaada inayotolewa na Jumuia ya Umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa makubaliano ya COTONOU hatua hii ya kuzishirikisha asasi zisizokuwa za kiserikali wakati wa kupitisha maamuzi imelenga kuongeza kasi ya maendeleo katika nchi hizo.

Nyuma ya wazo hili ni zana iliyojengeka kuwa asasi hizi zikiwezeshwa zina uwezo mkubwa wa kudhibiti vitendo vya rushwa na mianya mbalimbali ambayo hutumiwa na wanasiasa katika aidha kutumia vibaya misaada au kuingia mikataba mibovu na hivyo kuzitumbukiza nchi hizi katika madeni makubwa.

Kwa mujibu wa Umoja wa Ulaya hivi sasa watu bilioni moja katika nchi nyingi za ACP wanaishi kwa kutumia chini ya dola moja ya Marekani kwa siku. Wengi kati ya hawa wanaishi kusini mwa Jangawa la Sahara “ hali hii haivumiliki kwa Afrika na hata Ulaya” inasisitiza taarifa ya Umoja wa Ulaya.

EU lakini kwa upande mwingine inaonekana kuridhishwa na hatua za maendeleo zinazoanza kuchomoza hasa imani ya viongozi wengi wanaoingia madarakani kwa sasa. “ Afrika inapiga hatua. Afrika inabadilika haraka kwa kuvutia” inasisitiza taarifa ya EU.

Lakini suala la kuheshimiwa haki za binadamu, tawala za kidemokrasia na ustawi wa jamii yanazidi kuhimizwa.

Jambo lingine linalohimizwa na EU hasa kwa bara la Afrika ni Amani na usalama “ Umoja wa Ulaya EU utawasaidia wabia wake wa Afrika kuondokana na migogoro. mathalani mpango wa Amani wa EU kwa afrika, ambao hivi sasa umekuwa sawa na msingi wa kifedha kwa ajili ya kusaidia kujenga Amani na usalama”

“ Baadhi ya serikali za kiafrika zimeshakubali kufuatiliwa na chombo maalmu cha kuhakikisha kuwa yote hayo yanatekelezwa, kijulikanacho kama Afrika Peer Review Mechanism APRM ambacho ni chombo mahususi kwa ajili ya kutathmini na kujifunza”.

Hatua ya pili inayopendekezwa ni kukuza uchumi na biashara. Kuhakikisha kuwa umasikini unapungua kwa angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2015, na ili kufikia asilimia hizi basi angalau Afrika inapaswa kuhakikisha uchumi wake unakua kwa asilimia saba kwa mwaka.

Aliposimama kutoa neno la shukrani wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Bagamoyo Balozi wa Tanzani nchini Ubelgiji Saimon Mulai, alitaka kila upande yaani EU na ACP uangalie kwa kina kipi kinaweza kuboreshwa ili pande mbili za ushirikiano zinufaike.

Anakumbusha kuwa Nchi za Ulaya magharibi zimeendelea kwa kila hali, lakini pia akitaka isisahauliwe kuwa Umoja wa Ulaya unashirikiana na nchi dhaifu ambazo zilikuwa makoloni yake, hasa nchi kama Uingereza, Ujerumani Portugues nk.

Anatoa mfano kuwa ingawa EU imetoa soko wazi kwa bidhaa zinazotoka ACP lakini soko hilo lina viwango maalumu vinavyohitajika na masharti.

“ Huwezi kumkaribisha mgeni kwako ukampa nyama yenye mfupa na wewe unajua ana meno ya bandia ukamwambia bwana tafuna nyama” anasema Balozi Mulai.

Anasisitiza kuwa ili kuleta ushindani ulio sawa baina ya pande hizo mbili lazima nchi za ACP ziwezeshwe kwanza “ hatuna ule uwezo sasa tunatakiwa kuwezeshwa”.

Balozi Mulai anazigeukia pia nchi za ACP kuwa nazo hazijafanya vilivyo ili kunufaika kutoka nafasi zilizotolewa na EU.

“Lakini pamoja na kwamba tunasema tunatakiwa kuwezeshwa vile vile tunahitaji sisi kujiuliza tumejitahidi kiasi gani? Tumeelezea vipi mahitaji yetu na tumechangamkia vipi nafasi zilizopo?”, anahoji Balozi na kuonya.

“ no body should be left behind” , hakuna upande unaopaswa kuachwa nyuma kimaendeleo.

Anakariri maneno yaliyotumiwa na Balozi Baan wakati wa ufunguzi kusema “Tutaendelea safari yetu kwa pamoja”.

Anadadisi watu wanaweza kusafiri pamoja tena katika chombo kimoja lakini kwa madaraja (classes) tofauti na hata manufaa ambayo wasafiri hunufaika wawapo kwenye vyombo hivyo ati kwa sababu mmoja kaka daraja la kwanza, wengine la pili na la tatu.

“ Na hili ni jambo linatokea hata kama unasafiri kwa ndege, halafu unashangaa ikiwa nyote mwaingia kwa kupitia mlango ule ule, na kutokea mlango ule-ule mnaondoka muda ule ule na hata mnafika muda ule ule, lakini mnalipa nauli tofauti na madaraja tofauti”, anasema balozi Mulai na kuongeza

“ ni ushirikiano ndio, (wa EU na ACP) lakini ni ushirikiano ambapo lazima uelewe nafasi uliopo, na ufanye kile unachopaswa kufanya ili uweze kujipakiza kwenye chombo hicho kwa muda unaotakikana na kuteremka muda mwafaka ukiwa tayari umenufaika”.

Ushirikiano baina ya nchi za ulaya na ACP kimsingi ulianza mwaka 1975 kwa kutiwa saini makubaliano yaliyojulikana kama makubaliano ya Lome ambao ni mkataba wa kwanza katika mlolongo wa makubaliano ya ushirikiano yaliyofuata.

June mwaka 2000 nchi za ACP na Jumuiya ya nchi za ulaya zilikamilisha mkataba mpya wa ushirikiano wa miaka 20 uliojulikana kama Mkataba wa Cotonou. Mkataba huu ulianza kufanya kazi mnamo mwezi Aprili mwaka 2003.

Tanzania ambayo ni moja ya nchi za ACP tayari imenufaika sana na misaada mbalimbali kutoka EU.

Katika kipindi cha mwaka 2005 Umoja wa ulaya umetoa takliban Euro milioni 140, ambazo ni sawa na shilingi bilioni 200 za Tanzania.

Euro milioni 33.0 zililenga kusaidia mpango wa kupunguza umaskini na mango wa kurekebisha mfumo wa kiutendaji serikalini kama inavyoainishwa katika mpango wa MKUKUTA.

Euro milioni 62 kwa ajiri ya kusaidia miundombinu kama vile barabara nk, Euro milioni 44 kwa ajiri ya kusaidia elimu.

Hii ni pamoja na pesa hizo kusaidia nyanja mbalimbali kama vile mfuko wa kuinua hali za walikuma nchini STABEX.

Lakini pia EU imetoa Euro 14 milioni kwa ajili kuwawezesha wakimbizi 400,000 kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC Burundi na Rwanda waliokuwa wakiishi Tanzania kurudi makwao.

Mwisho.