1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa iko katika mtanziko juu ya mzozo wa Darfur

Josephat Charo23 Machi 2007

Wanasiasa na wanadiplomasia ulimwenguni kote wanatafuta suluhisho la mzozo wa Darfrur nchini Sudan. Jana bunge la Ujerumani Bundestag lilikutana kujadili mzozo huo na leo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, anatarajiwa kuzungumzia mzozo wa Darfur katika ziara yake nchini Misri.

https://p.dw.com/p/CHHb

Vifo takriban laki mbili na wakimbizi milioni mbili unusu ndio matokeo ya mzozo wa miaka minne katika jimbo la Darfur nchini Sudan. Serikali ya Sudan na jumuiya ya kimataifa zinabeba dhamana kwa kutopatikana suluhisho la mzozo huo. Mpaka sasa hakuna dalili ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya waasi na wanamgambo wa janjaweed. Majeshi ya Umoja wa Afrika bado hayana nguvu za kuuzima mzozo wa Darfur na jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani katika eneo hilo lilikataliwa na serikali ya Sudan.

Utawala wa Sudan hautaki amani na unabakia kulaumiwa kwa janga la Darfur. Hayo yalisemwa hivi majuzi na Minni Minnawi, kiongozi wa kundi kubwa la waasi huko Darfur, kundi pekee lililosaini mkataba wa amani na serikali ya Sudan. Kwa hatua hiyo Minnawi alipewa cheo serikalini mjini Khartoum na akawa na matumaini suluhisho lingepatakina kwa ushirikiano.

Sasa anasema kama serikali ingetaka, ingeweza kuumaliza mzozo huo. Mbali na hayo, Minnawi anasema ametengwa mjini Khartoum ambako hakuna anayemsikiliza, na Darfur ambako wapiganaji wenzake wamemgeuzia mgongo.

Makubaliano yake na utawala wa rais Omar el Bashir na ahadi zake hazikuwa na maana yoyote. Ukichunguza utaona rais Bashir ametoa ahadi nyingi kwa jumuiya ya kimataifa inazotaka kusikia. Lakini ukweli ni kwamba anazivunja ahadi zake zote. Kwa hiyo mambo hayaendelei vizuri.

Wasiwasi mpya unaosababishwa na rais Bashir ni kutorushu watu kujionea hali ilivyo katika jimbo la Darfur. Iwe ni vyombo vya habari, mashirika ya kutetea haki za binadamu na mashirika ya Umoja wa Mataifa. Amekataza visa za kusafiria. Aliamuru mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yasitishe kazi yao mwishoni mwa mwezi uliopita, hatua ambayo ilisababisha wasiwasi katika shirika la watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, na shirika la mpango wa chakula duniani.

Tatizo kwa hiyo sio eti jumuiya ya kimataifa haijakuwa wazi vya kutosha kuhusu mzozo wa Darfur. Swali ambalo si lazima liwe na jawabu ni kwamba inawezakana vipi serikali ya rais Omar el Bashir kutumia mamlaka yake kufanya inavyotaka? Swali hili limeelekezwa kwa jumuiya ya kimataifa. Mzozo wa Darfur unadhihirisha kwa uzito wote vipi jumuiya ya kimataifa ilivyo katika mtanziko.

Na majirani wa kiarabu wa Sudan wanafanya nini? Wanahofu Sudan huenda ikatumiwa kama mahali pa wanamgambo kujikusanya kama vile nchini Irak. Kama vita vya Irak au umwagikaji damu nchini Lebanon haungetokea, pengine ingekuwa kazi rahisi kwa majirani hao pamoja na mataifa ya magharigi kuibinya serikali ya Khartoum. Lakini kwa sasa wanafanya siasa za ndani. Hiyo ina maana wanazungumza maneno matupu dhidi ya mataifa ya magharibi na kumuacha rais Omar el Bashir afanye atakavyo.

Wakaazi wa Darfur ndio wanaolipa kutumia fedha zinazopatikana kwa umwagaji damu. Wanateseka chini ya dikteta katili, lakini pia kwa sababu ya unyonge wa jumuiya ya kimatafa inayoyasikiliza mataifa ya magharibi hususan Marekani. Maslahi ya muda na unafiki unazuia juhudi za kuishinikiza serikali ya Sudan.