1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa yafikiria vikwazo dhidi ya Korea ya kaskazini

10 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD4H

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa linafikiria kuweka vikwazo na mbinyu zinazofaa dhidi ya Korea ya kaskazini ambayo ililaumiwa kuwa iliripua bomu la kinyuklia chini ya ardhi. Tayari Marekani imependekeza vikwazo vya silaha na meli zote zitakazoelekea Korea ya kaskazini zipekuliwe.

Rais wa marekani George W. Bush alilaani vikali kitendo cha Korea ya kaskazini.

´´Tumekuwa tukiyachunguza madai ya Korea ya kaskazini. Lakini tayari madai kama yale ni pingamizi kwa amani na usalama duniani. Marekani inalaani vikali kitendo hicho cha uchokozi. Kwa mara nyingine tena, Korea ya kaskazini imepuuza jumuiya ya kimataifa na jumuiya ya kimataifa itachukuwa hatua´´.

Rushia na Uchina zimeitolea wito Korea ya kaskazini irejee kwenye meza ya mazungumzo na nchi 6 yaliyokwama. Wakati huo huo, aafisa moja wa Korea ya kaskazini ambae hakutajwa jina lake, ameliambia shirika la habari la Korea ya kusini la Yonhap, kwamba Korea ya kaskazini iko tayari kwa mazungumzo juu ya swala la silaha na vile vile iko tayari kuuacha mpango wake wa kinyuklia ikiwa Marekani itachukuwa hatua zinazostahili.

Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank Steinmeier, ameitolea wito Korea ya kakszini kutofanya jaribio jingine la kuripua bomu la kinyuklia.