1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa yalaani shambulizi Somalia

4 Desemba 2009

Umoja wa Afrika umeshutumu vikali shambulio la bomu la kujitoa muhanga ambalo limeuwa watu 19, ikiwa ni pamoja na mawaziri watatu wa serikali ya mpito nchini Somalia.

https://p.dw.com/p/Kq85
Majeruhi wa shambulio ya bomu jana nchini SomaliaPicha: AP

Wakati  huo  huo  msemaji  wa  kundi  kubwa  la  waasi nchini  Somalia  la  al Shabaab  amekana  leo   kuwa  kundi hilo  linahusika  na  shambulio  hilo.

p>Rais  wa   halmashauri   ya  umoja  wa  Afrika  Jean Ping ameshutumu  vikali  shambulio   hilo  lililotokea  jana .

Kitendo  hicho  cha  kinyama  ambacho  kinalenga  katika kuharibu  utaratibu  wa  kuleta  amani   hakitazuwia   umoja wa  Afrika  kutoa  msaada   kwa  serikali  ya  mpito  ya Somalia   kuleta  hali  ya  maridhiano  nchini  humo, imesema   taarifa  iliyotolewa  na  ofisi  ya  rais  wa halmashauri  hiyo .

UN Generalsekretär Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa UN Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/ dpa

Wakati  huo  huo  katibu  mkuu  wa  umoja  wa  mataifa Ban Ki-moon  na  baraza  la  usalama  la  umoja  wa mataifa   limeshutumu  vikali  shambulio  hilo.

Katibu  mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema   kuwa shambulio  hilo  litaimarisha  tu  nia  ya  serikali  ya Somalia   na  watu  pamoja  na  washirika  wengine kuendelea  na  juhudi  zao  za  kupambana  na  ugaidi nchini  Somalia.

Hili  amesema  katibu  mkuu  Ban Ki-moon  kuwa  ni shambulio  la  kihalifu  dhidi  ya   watu   ambao  wana nia ya   kuleta  maendeleo  kwa  njia  ya  amani.

Serikali  ya  Somalia  inayoungwa  mkono  na  umoja  wa mataifa   ya  rais  Sheikh  Sharif  Ahmed  inadhibiti   mitaa michache  tu  ya  mji  mkuu Mogadishu.

Siku  chache  kabla  ya  shambulio  la  jana  , wakaazi wamesema   kuwa   serikali  ilikuwa  inapanga  shambulio jipya  dhidi  ya   waasi.

Mkaazi  mmoja  wa  mjini  Mogadishu  Badra  Yussuf  Ali hata  hivyo  amesema  kuwa  jamii  imeingiwa  na  hofu kubwa  kutokana  na  shambulio  hilo la  kujitoa  muhanga.

Hali  kwa  sasa  iko  shwari  na  hata  hoteli  palipotokea shambulio  hilo  ni  shwari. Watu  bado  wana  majonzi baada  ya  shambulio  hilo  na  kuna  hali  ya  taharuki katika  jamii.

Waziri  wa  afya  wa  Somalia  Qamar  Aden  Ali, waziri  wa elimu  Ahmed Abdulahi  Waayeel  na  waziri  wa  elimu  wa juu Ibrahim  Hassan Addow  waliuawa  katika  shambulio hilo.

Waziri  wa  michezo Saleban  Olad Roble  amejeruhiwa  na yuko  katika  hali  mbaya.

Wakati  huo  huo  msemaji  wa  kundi  la  wapiganaji  wa al- Shabaab  amekana  leo  kuwa  kundi  hilo  limehusika katika  shambulio  hilo  la  hapo  jana.

Wanafunzi  pamoja  na  wazazi  wao  ni  miongoni  mwa watu  waliouwawa  katika  shambulio  hilo.

Msemaji  wa  Al-Shabaab  Sheikh  Ali  Mohammed   Rage amewaambia  waandishi  habari  kuwa  kundi  hilo halikuhusika  na   shambulio  hilo.

Amesema   kuwa  kundi  hilo  linaamini  kuwa   huenda  na njama  iliyofanywa  na   serikali  yenyewe.

Ameongeza Rage  kuwa  hiyo  si  katika  utaratibu  wa kundi  la  al Shabaab  kushambulia  watu  wasio  na  hatia. Rage  amesema   kuwa  mgawanyiko  mkubwa  wa  kisiasa umejitokeza  kati  ya  viongozi  wa  juu  wa  serikali  katika serikali  ya  rais  Sheikh Sharif  Ahmed  mjini  Mogadishu. Amedokeza   kuwa  tunafahamu  baadhi  ya  maafisa  wa serikali  waliondoka  katika  eneo  hilo  dakika  chache kabla   ya  shambulio. Na  hii  inaonyesha  kuwa wanahusika  na  shambulio  hilo.

Mwandishi:Sekione Kitojo

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman